Jumanne, 27 Desemba 2016

Ubingwa sio lengo la Azam kwenye michuano ya Mapinduzi Cup Afisa Habari wa Azam FC Jafar Idd amethibisha ushiriki wa klabu hiyo katika michuano ya Mapinduzi Cup inayotarajia kuanza December 30 hadi January 13 visiwani Zanzibar. Jafar Idd ametaja malengo ya mwalimu wa timu yao kushiriki michuano hiyo ambayo lengo lake ni kuadhimisha kumbukumbu ya Mapinduzi ya Zanzibar kila Jarury 12. Maandalizi ya michuano ya kimataifa “Ni michuano ambayo kwetu sisi Azam FC tunaiona dhahiri shahiri kwamba ni sehemu yetu ya maandalizi ya michuano ya kimataifa na mwendelezo wa ligi kuu Tanzania bara ambao tunaendelea nao sasa hivi.” Kujaribu wachezaji wapya “Kuna baadhi ya wachezaji ambao tumewasajili msimu huu kutoka nje ya nchi na wengine wakiwa ni wa hapa nyumbani, kwahiyo itakuwa ni changamoto yao kuonesha uwezo wao katika michuano hii ya Mapinduzi Cup.” “Tupo kundi moja na Yanga na hii ni mara ya pili mfululizo inatokea tunakutana nao kwenye kundi moja, tunaamini kuwa kundi letu litakuwa ndio lenye ushindani mkubwa, kila mtu anafahamu kuwa tunapokutana na Yanga aina ya mpira inakuaje na presha inakuaje kwa mashabiki, kwa hiyo ni matarajio yetu kutakuwa na ushindani mkubwa”. Katika malengo yote yaliyotajwa na Jafar Idd, hakuna lengo la kutwaa ubingwa wa michuano hiyo ambapo Azam ni washindi mara mbili wa kombe hilo ((2012, 2013). Azam FC ipo Kundi B, kundi moja na Yanga, Zimamoto na Jamahuri, Azam itacheza mechi yake ya kwanza Januari 2 kwa dhidi ya Zimamoto kwenye uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni