pata dondoo mbalimbali za michezo ya ndani na nje ya nchi.mompondazy itakujuza kila kitu.
Jumamosi, 24 Desemba 2016
Ngumu Kumeza kwa TFF ya mwaka 2016 madudu matupu... Naingia bar moja karibu na makaburi ya Kinondoni nakutana na jamaa mmoja, anaponiona anaropoka kwa nguvu akisema, umechelewa kidogo sana, ungekutana na wanaodogodesha mpira hapa nchini walikuwepo hapahapa. Namwambia kaka fafanua kauli yako umenitesa kimsamiati na ubongo wangu hauna shahada ya unyambuzi wa Kiswahili kama Omni Sigala. Ananiambia, namaanisha kuwa Rais wetu wa TFF inayozorotesha soka, alikuwepo hapa muda mfupi uliopita. Alikuwa na kiongozi wa Mbeya City pamoja na Zahoro Pazi, jamaa anaendelea kusema unajua lile suala alipaswa kuwajibishwa mtu lakini kwa vile uchaguzi upo karibu, watu wanafunika kombe mwanaharamu apite. Pengine ungeona afisa wa TFF akiwajibishwa kwenye issue ya Zahoro kama Kaijage na CD ya wimbo wa Taifa, nilitegemea kuona ukakamavu wa ufatiliaji wa vibali vya wachezaji wa kigeni kama wanavyofanya kwenye sheria na kanuni za mikoa lakini TFF ndio wamekuwa wa kwanza kuharibu taratibu za nchi kwa kuwapa leseni wachezaji wa kigeni. Nawaza tu, ingekuaje kama hawa wachezaji wa kigeni wangetenda kosa la jinai kwenye nchi hii na huku wanaishi kinyume cha sheria? TFF mngetokea wapi? Mbona hamjifunzi kupitia suala la Farid Musa ambaye amechelewa kujiunga na timu yake ya Hispania kwa kukosa kibali cha kufanyia kazi huko? Nikamwambia, wewe hayo yote umeyajua vipi? Akaniambia, mimi najua siri nyingi za TFF tangu nilipogundua Rais hana ofisi, nikigundua amekaa sehemu basi naagiza juice na kukaa nyuma ya kiti chake nasikiliza sana story zao kupitia hotel na bar. Jamaa anasema, unajua Rais anamfanya Katibu asiwe na kazi pale ofisini kwa vile anahodhi madaraka yote kama Mfalme Juha au Bi. Kilembwe wa pale Kiningi. Kama suala la Zahoro, kwanini asingemuachia Katibu, yule Katibu ananung’unika ndani kwa ndani. Ujue ngozi na nguo vinaficha vitu vingi sana, TFF kuna matatizo makubwa na ndiyo maana wanakuwa sehemu ya dhambi ya wachezaji wa kigeni pamoja na vilabu vyao. Nikisema TFF sio wazalendo nadhani utanielewa, usikute toka enzi za kina Wiliam Fanbulla, Ptrick Katalay, Pitchou Kongo, Nonda Shabani, Davis Mwape, Issa Abushir, Mark Serengo, Jama Mba, Patrick Ochan, Daniel Akufoh, Felix Sunzu, Pape Ndaw, Kiongera, Majwega, Sserunkuma, hadi leo wakina Twite, Angban na Mugiraneza usishangae wengi wao hawakulipiwa vibali na bado waliishi nchini. Kinachoangaliwa na TFF ni zile dola 2000 za maendeleo ya michezo na sio usalama wa nchi, mimi nilitamani Uhamiaji wangewakamata maafisa wa TFF waliotoa leseni kwa wachezaji wa kigeni kucheza bila vibali. Maana hawa ndio walioruhusu uozo wote huu utokee, wasingekuwa Ndanda kuzitaka zile pointi tatu kutoka kwa Simba, leo hii tusingesikia kitu. Kama wahamiaji wanaoingia kinyume na taratibu za nchi na aliyewaingiza au kuruhusu mchakato wao wa ajira huwa wanachukuliwa hatua za kisheria, Wizara ya Kazi na Uhamiaji vipi kuhusu hili? Mwandishi Mark Twain aliwahi kusema, Uzalendo ni kuiunga mkono nchi yako na serikali kwa muda wote kama inastahili. Hapa TFF ilistahili kuonesha Uzalendo jamani, anatokea muhudumu anatuletea vinywaji na yeye anatuhamisha kwenye ile mada kwa kusema, unajua tunavyowaambiaga Manji ni mkubwa kuliko Akilimali mlibisha, mnaona alivyotutetemesha kwa kuzima simu ndio maana timu ilianzisha mgomo baada ya kucheleweshewa mishara yao? Namwambia, issue sio ukubwa wa akili nyingi au udogo, issue pale ni nani wa kuhoji pesa za udhamini wa Quality Group kwenye jezi ya Yanga? Huyu ndiye anayekosekana. Angetokea Hawafu mwenye nguvu akaona umuhimu wa kuhoji, leo hii mngeweza kupata fedha kupitia jina la Quality. Sasa hoji uitishiwe Mkutano Mkuu wa Dharura ufukuzwe wewe na wanaokuunga mkono. Mhudumu anasema, unajua kwenye hili nimekuelewa sana. Kweli Quality haijawahi kutangazwa imeingia mkataba na klabu kwa muda gani, hivi zile pesa za haki za matangazo ya television kwenye huu mwezi ambao Mwenyekiti kavurugwa na Majembe, si ndio zingesaidia kulipa mishahara? Jamaa anamwambia, tatizo mnakuaga na nguvu ya kupiga kelele nje ya mikutano, mkiingia ndani chochote anachosema Mwenyekiti, mnasema sawa. Mnatamani hata akipiga chafya mpige makofi. Jamaa anasema, nilishangaa niliposikia wachezaji wamegoma kufanya mazoezi akiwemo Zulu. Sasa Zulu amegoma anadai kitu gani? Anaingia mchezaji mmoja wa Yanga anatuambia, jamani mimi mwenzenu katika kipindi hiki cha mgomo kiukweli kabisa toka moyoni nilikumbuka ile siku watu walipoingia bure uwanjani natamani yale mapato tungeyachukua.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni