pata dondoo mbalimbali za michezo ya ndani na nje ya nchi.mompondazy itakujuza kila kitu.
Jumatano, 21 Desemba 2016
MGOMO WA WACHEZAJI WA YANGA UNAVYOWEZA KUONYESHA KIASI GANI TUNAWEZA KUUSAHAU UBINADAMU KWA KOSA MOJA TU! Wachezaji wa Yanga, jana na juzi waligoma kufanya mazoezi ya timu yao kwa kuwa wamecheleweshewa kulipwa mishahara yao. Hii si mara ya kwanza kwa wachezaji wa Yanga kufanya hivyo, lakini safari hii wamefanya hivyo kwa siku mbili mfululizo. Wachezaji wa Yanga ni binadamu kama wengine. Wangependa kufanya matumizi yao na kadhalika, tena ukizingatia hiki ni kipindi cha sikukuu za Krismasi na mwaka mpya. Kawaida nao wangependa kufurahia na familia zao. Kama binadamu, kila mmoja angependa kuona familia yake ikiishi kwa amani. Katika hilo, ni jambo ambalo unawaelewa. Lakini kama nilivyowahi kusema awali, narudia leo tena kuwa kokote tunapotenda kazi, suala la ubindamu linatakiwa kuwa mbele yetu na ikishindikana hivyo, basi liwe ndani ya mioyo yetu kuamini wanaokuongoza nao ni binadamu na wanaweza kuwa na matatizo. Niliwahi kulizungumzia hili wakati wachezaji wa Simba, ikiwa mwishoni kabisa mwa msimu, wakagoma kwenda Songea timu ikisafiri kwenda kucheza na Majimaji, eti walicheleweshewa mshahara kwa siku 18. Leo Yanga, nao wamegoma baada ya kucheleweshewa mshahara kwa siku 19 na baadaye 20. Unaona kabisa kwamba wachezaji ni watu ambao wana upungufu na ambao mimi niwe wazi, siwaungi mkono kuingia kwenye upuuzi wa namna hiyo. Wewe unayesoma, kama ni mfanyakazi, umewahi mara ngapi kucheleweshewa mshahara na kuendelea kufanya kazi kwa mwezi mzima? Wachezaji wa Yanga, mara ngapi wamewahishiwa mshahara na wakashindwa kufanya kama ambavyo uongozi ulikuwa ukitaka na wala hawakulalamikiwa? Au wachezaji mara ngapi wamelipwa kwa kuwahishiwa na mara ngapi wamelipwa kwa kucheleweshewa? Hapa suala la busara ndiyo lilipaswa kuongoza. Maana kama watalipwa leo, zile siku walizogoma inakuwaje? Watazilipa vipi? Katika malipo ya mwezi ujao, nazo zilipwe au zikatwe kwa kuwa hawakufanya kazi? Je, wachezaji wa Yanga wanajua mwenyekiti wao ni binadamu? Huenda alikuwa katika misukosuko ya kibinadamu, hivyo ikashindikana kuwalipa kwa wakati mwafaka? Au wanajua wadhamini wao wako katika misukosuko, inaweza kuwa chanzo cha kuwacheleweshea kwa siku 20 na ingewezekana kupambana kwa njia ya amani na mwisho wakalipwa? Lakini najiuliza, kumbe wachezaji wa Yanga hawana akiba, wasipolipwa kwa siku 20 hawawezi kuishi? Unataka kuniambia wachezaji wa Yanga hawana mapenzi na klabu hiyo zaidi ya mishahara yao? Kwamba mshahara ukikosekana kwa siku 20, wao nguvu zinaisha? Ni kweli wachezaji wote wa Yanga wamegoma au wengine ni bendera fuata upepo na kwa nini wanapelekwa tu? Uongozi wa Yanga unapaswa kutokaa kimya katika hilo, badala yake uchukue hatua kwa vinara na kuwaonyesha kuwa katika maisha wakati mwingine kuna nafasi ya kuvumiliana. Mimi ninaunga mkono wachezaji kulipwa maslahi yao, tena ikiwezekana ni vizuri walipwe mapema kwa sababu ya kuwapandisha morali katika kazi zao kwa kuwa kweli ni ngumu. Lakini bado ninaamini, hata wao wachezaji wanapaswa kuwa na busara, kujua kuna shida na wakati mwingine suala la kuchelewa kulipwa linaweza kutokea, hasa kama si jambo la mara kwa mara. Wasiwe ni watu wenye papara, fuata mkumbo au mihemko, wakati mwingine hata kama kuna shida, busara ni jambo jema. Jiulize ikitokea Yanga ikashindwa kufanya vizuri katika mechi dhidi ya Lyon, watajisikia vipi au watafanyaje na wanaweza kueleza vipi? Kocha George Lwandamina ameonekana kukerwa na hilo. Ingawa hajaenda moja kwa moja, ujumbe wake kwenye Mtandao wa Facebook jana, unaonyesha wazi hisia zake kwamba ameona hiyo si nidhamu bora. Ameeleza namna mtu anavyoweza kulitanguliza suala la nidhamu. Hakufunguka wazi, huenda kutokana na ugeni wake lakini anaamini kwamba wachezaji wangeendelea na majukumu yao wakati suala hilo linashughulikiwa. Kama unakosewa leo, vizuri kukumbuka na mazuri mengi mliyofanyiwa nyuma kabla ya leo kukosewa. Wachezaji lazima wajue, hawaongozwi na malaika na tukubali, siku 20 hazitoshi kusababisha mgongano kwa kuwa bado watu wanakuwa na nafasi ya kuvumilia na busara inakuwa na nafasi ya kutozidiwa nguvu na mihemko. Kweli wachezaji mnategemewa, kweli ni watu muhimu sana. Lakini kumbukeni wanaowaongoza pia si malaika, ni watu kama nyie na ikiwezekana kunapokuwa na sehemu ndogo wamekosea, kwanza mjiulize kwa nini na mfanyeje kurekebisha badala ya kutanguliza papara, kama si mshahara kuna kingine mkiseme. SOURCE: CHAMPIONI
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni