Jumatano, 26 Oktoba 2016

Yanga bila Pluijm yawakalisha wanajeshi

Mechi ya kwanza bila kocha wao mkuu, kikosi cha Yanga kimepata ushindi wa bao 4-0 dhidi ya JKT Ruvu Stars ikiwa ni mwendelezo wa ligi kuu Tanzania bara. Kocha msaidizi Juma Mwambusi alisimama kwenye benchi la ufundi kutokana na aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo Hans van Pluijm kujiuzulu kuifundisha timu hiyo. Obrey Chirwa ameendeleza moto wake wa kufumania nyavu baada ya leo kupachika bao la kwanza dakika ya 6 lililoipa Yanga uongozi wa katika mechi hiyo hadi kipindi cha kwanza kinamalizika. Mrundi Amis Tambwe alifunga bao la pili dakika ya 63 kabla ya Simon Msuva kuifungia Yanga goli la tatu dakika ya 83. Tambwe alifunga goli la nne dakika ya 90+2 likiwa goli lake la pili kwenye mechi ya leo na kuhitimisha kipigo kingine siku chache baada ya kuishinda Kagera Sugar kwa goli 6-2 ugenini kwenye uwanja wa Kaitaba, Kagera. Dondoo Yanga imeshinda JKT Ruvu kwa magoli manne katika mechi tatu za mwisho. Yanga imefunga magoli 10 katika mechi mbili za mwisho. Kagera Sugar 6-2 Yanga na Yanga 4-0 JKT Ruvu Stars. Wafungaji wa magoli ya leo jezi zao zina namba saba mgongoni. Obrey Chirwa (7), Simon Msuva (27) na Amis Tambwe (17). Tambwe, Chirwa na Msuva tayari wameshafunga magoli 16 hadi sasa. Tambwe (6), Chirwa (5) na Msuva (5). Obrey Chirwa amefunga magoli matano katika mechi alizocheza. Amefunga mfululizo kwenye mechi tatu za mwisho. Alianza kunga kwenye mchezo wa Yanga 3-1 Mtibwa, mchezo wa Azam vs Yanga hakufunga ulimalizika 0-0, akafunga kwenye mechi ya Toto Africans 0-2 Yanga, Kagera Sugar 2-6 Yanga na leo October 26 Yanga 4-0 JKT Ruvu Stars. JKT Ruvu imepoteza mfululizo mechi zake tatu za mwisho, ilifungwa na Ruvu Stars 0-1 Kagera Sugar, Azam FC 1-0 JKT Ruvu na Yanga 4-0 JKT Ruvu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni