Mshambuliaji wa Simba, Frederic Blagnon raia wa Ivory Coast, amepewa mapumziko ya siku saba kutokana na majeraha ya kuchanika juu ya jicho aliyoyapata wikiendi iliyopita kwenye mchezo dhidi ya Toto Africans uliopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0, Blagnon aligongana na beki wa Toto, Yusuf Mlipili hali iliyomfanya ashindwe kuendelea na mechi hiyo na nafasi yake kuchukuliwa na Laudit Mavugo.
Daktari wa Simba, Yassin Gembe, amesema walilazimika kumshona nyuzi nne kutokana na majeraha aliyoyapata, lakini kwa sasa anaendelea vizuri.
“Kwa sasa Blagnon anaendelea vizuri baada ya kupata majeraha juu ya jicho ambapo tulimshona nyuzi nne, tumempa mapumziko ya siku saba ili apone kabisa, hivyo ana asilimia ndogo ya kusafiri na timu kwenda Shinyanga,” alisema Gembe.
Kwa upande wake Blagnon alisema kuwa: “Namshukuru Mungu naendelea vizuri, kilichotokea siku ile ni sehemu ya mchezo na siwezi kumlaumu mpinzani wangu, nawatakia kila la heri wenzangu huko waendako warudi na ushindi ili safari yetu ya ubingwa isiingie doa.”
Simba jana Jumanne ilitarajiwa kwenda Shinyanga kwa usafiri wa ndege kucheza mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mwadui utakaopigwa Jumamosi hii na dhidi ya Stand United Jumatano ijayo. Mechi zote hizo zitapigwa kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani humo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni