Na Saleh Ally KAMA Kocha Juma Mwambusi angeanza na mshambuliaji Amissi Tambwe katika mechi dhidi ya JKT Ruvu, hakika habari ingekuwa nyingine kabisa. Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda kwa mabao 4-0, lakini Donald Ngoma, Obey Chirwa, Thabani Kamusoko na Simon Msuva walipoteza zaidi ya nafasi sita za wazi za kufunga. Tambwe ni muuaji unapozungumzia suala la kufunga, hataki utani na katika nafasi nne anaweza kupoteza moja na kufunga tatu. Hakika ni kati ya washambuliaji wenye kipaji cha juu cha kufunga au umaliziaji. Wakati Ligi Kuu Bara msimu wa 2016-17 inaanza, ilionekana kama vile makali yake yameisha licha ya kwamba katika misimu miwili iliyopita tayari alikuwa mfungaji bora mara mbili. Na msimu mmoja akawa katika nafasi ya pili. Kocha Hans van der Pluijm amerejea Yanga baada ya uongozi wa klabu hiyo, kuukataa uamuzi wake wa kutangaza kujiuzulu. Maana yake bado Tambwe ana nafasi ya kuendelea kufanya vema kama ataendelea kumpa nafasi ya kutosha. KICHUYA Kwa sasa Tambwe anaonekana kuwa katika kiwango bora zaidi baada ya kufikisha mabao matano kwa mabao aliyofunga katika mechi tatu tu za ligi. Alianza Septemba 10 wakati Yanga ilipoitwanga Majimaji kwa mabao 3-0, yeye akafunga mawili. Septemba 17, Yanga ikiwa ugenini mjini Shinyanga ikashinda kwa mabao 2-0, Tambwe tena akafunga na kuonyesha si mtu wa mchezomchezo. Oktoba Mosi, akafunga bao dhidi ya Simba ambalo lilizua utata mkubwa. Baada ya hapo, mwendo wake ukawa wa kusuasua hasa baada ya kuumia. Lakini aliporejea, mechi ya kwanza aliingia dhidi ya Kagera Sugar, Yanga ikishinda kwa mabao 6-2, hakufanya lolote. Mechi iliyofuatia dhidi ya JKT nayo aliingia akapachika mabao mawili ya haraka na kusaidia ushindi wa mabao 4-0. Sasa Tambwe ana mabao sita, moja pungufu dhidi ya kinara wa ufungaji mabao kwa sasa. Huyu ni Shiza Kichuya, Mtanzania pekee anayeonekana kuwa na kasi kubwa katika ufungaji wa mabao. Kichuya ameiongoza Simba vema na ilionekana kasi yake ni gumzo, lakini mwendo wa Tambwe tayari umezua hofu na huenda unaweza kusababisha Kichuya kutotulia kama asipousoma mchezo mapema. Kwamba bado anatakiwa kusaidia zaidi kuliko kufunga. Katika upachikaji mabao, Tambwe ni ‘Mnyama’, hataki utani na anapoingia uwanjani anataka kufunga kweli. Kinachomsaidia, silaha tatu za mfungaji mahiri anazo. Yaani ana uwezo wa kutumia vizuri mguu wa kulia, anaweza kufunga kwa kushoto, halafu ni mshambuliaji hatari zaidi anayeweza kufunga mabao ya vichwa. Rekodi za nyuma zinambeba Tambwe kama mshambuliaji hatari zaidi kwa misimu yote mfululizo. Kwa kuwa amekuwa mfungaji bora mara mbili, mara moja kashika nafasi ya pili. Utaona katika Ligi Kuu Bara kwa misimu mitatu na robo, tayari amepachika mabao 60 katika ligi tu, huyu si mtu wa kawaida na kupambana naye inatakiwa ubunifu mkubwa na nidhamu ya hali ya juu. Mabao 19 alifunga katika msimu wa kwanza akiwa Simba, akaibuka kuwa mfungaji bora, msimu uliofuata, bao moja akafunga akiwa Simba, 13 akafunga akiwa Yanga na kumaliza msimu akiwa na mabao 14 na msimu uliopita akawa mfungaji bora tena akiwa mabai 21. Msimu huu ambao kwake amecheza robo ya msimu ambao mechi hadi saba, tayari ana mabao sita na kama hajaumia, hakika ataendelea kufunga zaidi. Katika misimu yote mitatu, kila mmoja alipiga hat trick moja au mbili. Hajafanya hivyo msimu huu na inaonekana kwa anavyokwenda kuna uwezekano mkubwa wa kufanya hivyo. Nimekuwa nikieleza kila mara, kwamba Tambwe ni mchezaji tofauti kabisa kati ya wengi waliowahi kucheza soka nchini. Pamoja na kuwa na kipaji cha juu, lakini ana nidhamu ya juu pia. Kuweka kipaji bora na nidhamu sahihi, hakika jibu ni maendeleo. Hiki ndicho kitamsaidia na inawezekana ikawa ni vigumu au kazi ngumu sana kwa Kichuya kupambana na Tambwe hasa ukizingatia sasa anaonekana kuwa ‘on fire’. Kama Kichuya atanuia na kupambana naye, itakuwa ni changamoto na mafunzo makubwa yanayoweza kuinua kiwango chake zaidi katika ufungaji kuliko alivyo sasa. Tambwe: 2013/14 mabao 19 2014/15 mabao 14 2015/16 mabao 21 2016/17 mabao 6 MECHI ALIZOFUNGA MSIMU HUU… 2016/17 Septemba 10, 2016 Yanga 3-0 Majimaji FC Taifa Kaseke 19 Tambwe 79 Tambwe 84 Septemba 17, 2016 Mwadui FC 0-2 Yanga Kambarage Amissi Tambwe 5 Donald Ngoma 94 Oktoba 1, 2016 Yanga 1-1 Simba Taifa Tambwe 26 Kichuya 87 Oktoba 26, 2016 Yanga 4-0 JKT Ruvu Taifa Obrey Chirwa 6 Amissi Tambwe 63 Simon Msuva 82 Amissi Tambwe 90
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni