pata dondoo mbalimbali za michezo ya ndani na nje ya nchi.mompondazy itakujuza kila kitu.
Jumanne, 25 Oktoba 2016
Hans van der Pluijm kwajinsi ulivyo wapa fulaa wana Yanga umewafanya wasiamini kocha mwengine umekua kama ‘mkuki’ ulioingia katika Vifua vya wana Yanga, kocha mpya apewe sapoti na kila mmoja…
Nani mshauri wa Yusuph Manji? Katika dunia ya soka ‘makocha wanaajiriwa na kufukuzwa, na wakati mwingine wanajiuzulu kwa sababu kadha wa kadha.’ Mfano ni Sir Alex Ferguson, yeye aliamua kustaafu ghafla kuinoa Manchester United, Mei 2013 kwa sababu za kifamilia.
Juppy aliamua kustaafu kazi ya ufundishaji baada ya kuiwezesha FC Bayern Munich kutwaa mataji matatu likiwemo lile la ligi ya mabingwa Ulaya Mei 2013.
Mjerumani huyu mshindi kiufundishaji alistaafu kwa sababu ya umri kumtupa mkono. Pia wapo makocha ambao hufukuzwa kazi, kwa sababu ya matokeo mabaya ya timu, pia wengine kwa sababu zisizo za kimpira.
Mfano wa makocha waliofukuzwa kazi ni Jose Mourinho. Mreno huyo aliondolewa Chelsea msimu uliopita kwa sababu za matokeo. Mbelgiji, Tom Saintfiet yeye alifukuzwa alikuwa kocha wa kwanza kufukuzwa kazi na Yusuph Manji mara baada ya tajiri huyo kukalia kiti cha uenyekiti wa klabu ya Yanga, Julai 2012.
Tom aliondolewa siku 76 baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili kuifundisha timu hiyo. Kilichomuondoa si sababu za kimpira kwa maana alikuwa ametoka kuipa Yanga taji la Cecafa Kagame Cup Julai, na aliisimamia timu hiyo katika michezo miwili tu ya ligi kuu Tanzania Bara msimu wa 2012/13.
Baada ya kuchapwa 3-0 na Mtibwa Sugar, Septemba 2012 katika game ya ufunguzi pale Jamhuri Stadium, Morogoro, Tom kama mkuu wa benchi la ufundi akarudisha timu yake jijini, Dar es Salaam licha kwamba Manji alitaka timu iende moja kwa moja jijini, Mbeya kwa ajili ya mchezo mwingine dhidi ya Tanzania Prisons.
Nakumbuka baada ya game ile iliyomalizika kwa sare pale Sokoine Stadium, Tom alisema hadharani jinsi wachezaji wake walivyolala wawili wawili katika kitanda kimoja na akaelezea kiufundi kama mwalimu kwamba hali hiyo ilivuruga utulivu na kubadilisha saikolojia ya wachezaji wake.
Kitendo cha kusema maneno hayo katika vyombo vya habari kulimuweka matatani kwa maana aliitwa na Manji na kupaswa kujieleza ni kwanini asifukuzwe kazi. “Mimi ni kocha, wewe ni mfanyabiashara, na si mfanyabiashara wa kimataifa, niache nifanye kazi yangu.” Ni maneno ambayo Tom alimwambia Manji baada ya mwenyekiti huyo kuchukizwa na kauli ya kocha huyo kusema hadharani jinsi wachezaji wake walivyotelekezwa wakiwa Mbeya.
Nilipinga sana kuondolewa kwa Mbelgiji huyo kwa sababu hapakuwa na sababu yoyote ya kimpira iliyofanya akaondolewa ndani ya miezi miwili na nusu klabuni hapo. Nafasi yake ilichukuliwa na Mholland, Ernie Brandts ambaye alifanikiwa kuwapa Yanga taji la VPL.
Brandts alijitahidi kuibadilisha Yanga kiuchezaji. Lakini baada ya miezi isiyozidi 18 naye akafukuzwa kazi na Manji kisa kuhoji sajili za Emmanuel Okwi na Juma Kaseja waliosajiliwa Yanga wakati wa usajili wa dirisha dogo mwezi Desemba 2013.
Brandts kama kocha alisema hakuwahitaji wachezaji hao katika kikosi chake na jambo hilo lilimkera Manji akaamua kumfuta kazi wiki moja baada ya kocha huyo kusaini mkataba mpya wa miaka miwili.
Hans van der Pluijm akachukua nafasi yake kwa mkataba wa miezi 6, lakini timu ilishindwa kutetea ubingwa wake wa VPL ambao ulikwenda kwa timu ya Azam FC msimu wa 2013/14.
Wengi waliamini, Hans angepewa mkataba wa muda mrefu kufuatia kiwango kizuri cha timu hiyo ndani ya utawala wake wa muda mfupi. Lakini akaamua kwenda barani Asia Manji akamshawishi kocha wa zamani wa Taifa Stars, Mbrazil, Marcio Maximo kurejea nchini kuinoa klabu yake.
Katikati ya mwaka 2014, Maximo alisaini mkataba wa miaka miwili lakini baada ya Yanga kuchapwa 2-0 na Simba SC mwezi Desemba katika game ya Nani Mtani Jembe, Mbrazil huyo naye akaondolewa na Hans akarejea tena katika klabu hiyo mwanzoni mwa mwaka 2015.
Alikuja Yanga akiwa mwalimu mwenye miaka 65. Umri ambao wakati mwingine watu husema ‘umepitwa na wakati’ katika soka la kisasa. Katika mchezo wa soka, ili kocha upate hamasa ya wachezaji, unahitajika kwanza kuwa na hamasa hiyo wewe mwenyewe. Kuwa na matarajio ya kufanikisha mipango mikubwa kama kocha husaidia kwani huwaingia wachezaji pia.
Ilikuwa kama njia ya Hans kuweka kiwango cha juu katika timu kwa ajili ya mafanikio ya siku za sasa na baadae. Hans alikuwa akifanya kazi yake kwa bidii, na mazoezi aliyofundisha yalikuwa na ubora labda kuliko yote waliyowahi kupata wachezaji wa Yanga.
Mara nyingi ari ikiwa hivyo katika timu huwa ni kipindi kizuri mno kwa wachezaji kukuza viwango vyao kiuchezaj. Hans hakuwa mtu wa kujijali mwenyewe bali yeye alikuwa na mtazamo wa timu na jinsi ya kuinua viwango vya wachezaji wake.
Yanga watamkumbuka, Hans na bila shaka mkufunzi huyo pia ataikumba Yanga timu ambayo imemtengenezea marafiki wengi wazuri kutokana na kazi yake aliyoifanya. Inaumiza kuona timu ikiachana na kocha aliyepoteza mechi mbili tu katika game 40 za ligi kuu.
Ni kweli mabadiliko ya makocha ni jambo la kawaida katika mpira lakini nadhani Yanga ilipaswa kuendelea na Hans walau hadi mwishoni mwa msimu huu. Jambo la kufanya kwa sasa ni wachezaji, wanachama, viongozi na mashabiki wa timu hiyo kujiandaa kumpa ushirikiano wa kutosha kocha ajaye ili aendeleze kile alichokiacha Hans.
Sapoti ni jambo muhimu litakalo mbeba mrithi wa Hans vinginevyo timu itakuwa imejirudisha hatua nyingi nyuma. Yanga hawawezi kumsahau Hans na ikitokea timu kufanya vibaya ndani ya uwanja watamkumbuka sana Mdachi huyo.
Kuondoka kwa Hans ni sawa na mkuki uliopenya katikati ya kifua cha wana Yanga lakini wanaweza kuendelea kuwa na furaha kama watakuwa upande wa kocha ajaye.
Tazama United inavyo safa bila Sir Alex, pia tazama mwenendo wa PSG bila Laurent Blac. Ila, Barcelona imeshamsahau Pep Guardiola. Kwa nini? Yanga wanapaswa kusahau kuhusu Hans na badala yake wamshukuru kwa kuifikisha timu yao ilipo sasa na kumuunga mkono kocha mpya japo inaumiza.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni