Jumatatu, 19 Septemba 2016

PLUIJM: NYIE TUKAMIENI TU LAKINI TUKIKUTANA, TUNAWAPIGA

Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans Pluijm, ameziambia timu pinzani kuwa ziendelee kuipania timu yake lakini zijue kuwa lazima zikumbane na kichapo tu mbele ya Yanga. Kauli hiyo aliitoa mara baada ya mechi dhidi ya Mwadui FC inayofundishwa na kocha, Jamhuri Kihwelo 'Julio' iliyomalizika kwa Yanga kushinda mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga. Yanga hivi sasa imefikisha pointi 10 sawa na Azam FC iliyofungwa na Simba juzi lakini Jangwani wapo nafasi ya pili wakiwa na uwiano mzuri zaidi wa mabao. Simba ndiyo inayoongoza ligi baada ya ushindi wa juzi. Akizungumza na Championi Jumatatu, Pluijm alisema hivi sasa anaingia uwanjani na tahadhari kwa lengo la kupata ushindi kutokana na kila timu anayokutana nayo kucheza kwa kuwapania kwa lengo na kutaka kuifunga Yanga.  Pluijm alisema yeye atakachokifanya hivi sasa katika mechi zake za ligi, ni kutoidharau timu yoyote na badala yake atapanga kikosi kitakachompa ushindi kuhakikisha anakaa kileleni kwenye msimamo wa ligi kuu. “Ujue hivi sasa kila timu inayokutana nasi inacheza kwa kutupania kwa maana ya kucheza kwa kujihami kwa kulinda goli lao huku wakicheza rafu za makusudi.  "Lengo lao ni kutaka kutufunga ili waweke historia, hivyo nimeliona hilo na nimepanga kulidhibiti kwa kukiandaa kikosi changu vema ili kuhakikisha tunawafunga mwisho wa mchezo. "Lakini napenda nichukue nafasi hii kuwapongeza wachezaji wangu kwa kucheza kwa kujituma kwenye mechi zetu nne tulizozicheza ambazo tatu tumeshinda na nyingine moja tumetoka sare na Ndanda FC,” alisema Pluijm. Juzi Yanga iliichapa Mwadui mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga kwa mabao ya Amissi Tambwe na Donald Ngoma. SOURCE: CHAMPIONI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni