Jumamosi, 24 Septemba 2016

OMOG AFUNGUKA KUHUSIANA NA SUALA LA OKWI KUREJEA SIMBA

Uongozi wa Simba unapanga kimyakimya kumrudisha kikosini kiungo mshambuliaji wake Emmanuel Okwi, lakini kocha wao Joseph Omog amedai hajui dili hilo na wala hana mipango naye. Simba inaamini Okwi anayecheza Klabu ya Sonderjyske ya Denmark ambayo alijiunga nayo msimu uliopita kwa dau la dola 120,000 (Sh milioni 250), akiungana na Laudit Mavugo na Ibrahim Ajib mambo yao yatakuwa mazuri. Omog alisema hajui lolote kuhusu dili la kumrudisha Okwi na hajaambiwa lolote na uongozi hadi sasa. “Sina taarifa zozote kuhusiana na mpango huo kwani sijashirikishwa, hivyo siwezi kusema chochote lakini pia mchezaji huyo simjui kabisa na wala sijawahi kumuona,” alisema Omog na kuongeza: “Kwa sasa sihitaji mchezaji yeyote katika kikosi changu kwani hawa waliopo wananitosha labda baadaye sana endapo nitaona kama kuna ulazima sana wa kuongeza mchezaji mwingine wa kigeni.” Habari za kuaminika kutoka Simba zinasema kama mambo yakienda sawa, Okwi raia wa Uganda, anaweza kusajiliwa katika usajili ujao wa dirisha dogo kuchukua nafasi ya Javier Bokungu raia wa DR Congo. SOURCE: CHAMPIONI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni