Kumekuwa na hofu kwamba Congo wanachezesha vijeba katika mechi zao za vijana chini ya umri wa miaka 17 kuwania kucheza Kombe la Mataifa Afrika. Lakini timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, iko tayari kwa kazi hiyo ngumu unayowezeka kuilinganisha na mzigo wa Mnyamwezi. Kesho Jumapili inacheza mechi muhimu ya kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Vijana 2017 dhidi ya Congo Brazzaville. Mchezo wa marudiano utachezwa kwenye Uwanja wa Alphonse Massamba Debat na katikati atasimama mwamuzi Pacifique Ndabihawenimana wa Burundi akisaidiwa na Pascal Ndimunzigo na Gustave Baguma. Serengeti Boys inayonolewa na Bakari Shime inacheza mechi hiyo baada ya awali kushinda mabao 3-2 nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa, na ikiitoa Congo itakuwa imefuzu kucheza fainali hizo za Afrika. Kikosi cha timu hiyo tayari kipo Congo baada ya kuwa kambini nchini Rwanda kujiandaa na mchezo huo. Serengeti ikifanya vizuri itafuzu kushiriki fainali hizo za 12 za michuano hiyo ya vijana. Fainali hizo zitashirikisha timu nane za Afrika wakiwemo wenyeji Madagascar na michuano imepangwa kuanza Aprili 2 hadi 16, 2017 katika miji miwili ya nchi hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni