Ijumaa, 23 Septemba 2016

KAZI IPO KWA WAYNE ROONEY, ANAKETI AU ANASIMAMA?

Kumbuka ile siku, siku muhimu sana kwenye maisha ya Wayne Rooney. Ni ile siku ambayo alinyanyuliwa kutoka kwenye benchi kijana mwenye umri wa miaka 16 tu chini ya kocha David Moyes kunko klabu ya Everton. Ilikuwa mchezo dhidi ya Arsenal ya mzee Wenger. Mpira ukiwa unaelekea mwisho, Moyes anampa nafasi kinda wa miaka 16 anaenda kuamua matokeo kwa goli la kiutu uzima lililomzidi miaka pengine 10. Ndio alifunga bao kwa shuti kali ambalo lilizoeleka kwenye miguu ya wanaume wenye miaka pengine 26 na kuendelea. Alikuwa ni Wayne Rooney huyu ambaye aliweza kwenda katika michuano ya Euro na kufanya maajabu kabla hajapata majeraha yaliyomfanya kutokuendelea na mashindano hali iliyopelekea Waingereza kuamini kuwa ni kinda huyu ndiye aliyesababisha wao kuondolewa mashindanoni kutokana na kuumia kwake. Hakuzungumzwa Gerrard, wala Owen na sio Beckham bali ni Wayne Rooney. Alizaliwa na nyota, akakua na nyota na akawa nyota ambayo kila mchezaji kinda au vijana wadogo walitamani kuwa. Mapafu ya mbwa ambayo yalimpa kiburi Sir. Alex Ferguson kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi nyingi kwa wakati mmoja. Alikuwa mchezaji aliyekamilika zaidi katika uso wa dunia katika wakati wake wa soka. Miaka imesogea sana. Imepita nyakati kadhaa, hawapo tena wachezaji wa aina yake, wabunifu kumzidi wamepungua na wagumu kama yeye hawapatikani. Bahati mbaya ni kuwa hata yeye mwenyewe anapotea na yupo hatarini kutoweka. Sio yule tena ambaye angeweza kukupa mabao 15 na pasi 10 kwa mwaka. Sio Rooney yule aliyewatisha mabeki kutokana na nguvu zake na akili kwa pamoja. Haonekani Roooney ambaye alibatizwa jina la “The White Pele” machoni kwa watu.Mwanzo ungeweza kuamini pengine nyakati za Moyes mpaka Van Gaal zilikuwa zinammaliza lakini hata huyu ambaye wengi wanaamini katika uwezo wake yaani Mourinho, hapati anachostahili kutoka kwa Rooney. Mourinho ni aina ya makocha ambao wangeweza kuendana sana na Rooney kwa maana ya kuweza kutumia nguvu zake na uwezo wake wa kukaba na kushambulia kwa wakati mmoja ila anaonekana sio yeye. Hafanani na Rooney aliyezoeleka na hata amri yake juu ya mpira haipo. Mpira haumtii kila anapouamrisha na bahati mbaya inaonekana hata misuli imeanza kumgomea. Mourinho anapata wakati mgumu kumuacha kikosini lakini anajua ukweli fika kuwa Rooney kwa sasa anajikaba mwenyewe huku akiikaba na timu yake pia. Wepesi wake umepungua hali inayomfanya kupunguza ubunifu, ujanja wake mbele ya goli umepotea na hata urafiki wake uliozoeleka na washambuliaji anaocheza nao haupo na anajikuta mkiwa muda mwingi. Timu inapocheza inajikuta imemtenga. Ni ajabu lakini kwa mara ya kwanza ninaweza kuwa ninashuhudia Mourinho ambaye ni mwoga. Sio Mourinho ambaye alimkata kichwa Iker Casillas na wala sio Mourinho ambaye alimwondoa Mata na akashinda ubingwa kuwanyamazisha waliopiga kelele dhidi yake. Huyu wa sasa anaonekana kuwa na imani na Rooney. Imani ambayo napata shaka kama itampeleka peponi au imamtupa motoni. Ni ngumu sana kwa sasa kupata ubora wa Rooney hasa namna ambayo presha kwa timu na wachezaji inaendelea kuongezeka. Kipindi ambacho ushindani kwenye ligi umeongezeka kwa maana ya idadi ya vilabu bora. Umefika wakati Rooney anatakiwa kuanza kutokea kwa nadra katika kikosi cha kwanza. Hii itamsaidia kurejesha nguvu yake, kupunguza presha na kuongeza ubunifu atakapohitajika. Tatizo sioni kama yupo tayari kwa huli na sijawaza namna ambayo Mourinho anamweka benchi. Rooney anahitaji pumziko, tatizo ni je yupo tayari kuketi au atang’ang’ania kusimama akipige uwanjani?

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni