Jumatatu, 26 Septemba 2016

Kumbe Azam fc kimenuka Ukweli huu apa ‘Kujiondoa katika timu kwa watoto wa mmiliki Azam FC ni tatizo…?’

Na Baraka Mbolembole ACHANA na vipigo viwili mfululizo ambavyo timu ya Azam FC imekumbana navyo katika ligi kuu Tanzania Bara msimu huu, ndani ya timu hiyo mambo si shwari kama ilivyokuwa misimu iliyopita kufuatia kuwapo kwa mgogoro kati ya mmiliki wa timu hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007 na baadhi ya watoto wake. Kilichotokea ni kwamba, baada ya mmiliki ‘kuwakaribisha’ baadhi ya watu wenye asili ya Asia ndani ya timu hiyo na kuwapa mamlaka makubwa, watu hao wakaanza kupeleka maneno kwa mmiliki wa timu na kumwambia kuwa vijana wake wanatumia vibaya pesa jambo ambalo liliwakera watoto hao baadhi na kuamua kujiweka kando. Kitendo cha kujiweka kando kwa vijana hao ambao wamekuwa na msaada mkubwa kwa timu hiyo tangu kuanzishwa kinadaiwa kuanza kutoa athari ndani ya timu kwa kuwa baadhi ya mahitaji ambayo yalikuwa yakipatikana klabuni hayapo tena na tayari ukata umeanza kupigiwa kelele ndani ya timu hiyo. Azam FC hadi wanatwaa taji lao la kwanza la VPL msimu wa 2013/14 ilijiwekea utaratibu wa kutoa posho kwa kila mfanyakizi pale Azam Complex, Chamanzi. Kwa mfano, timu ikishinda wafanyakazi wote walikuwa wakipatiwa posho ya juu na ikitokea matokeo ya sare ama kupoteza mechi posho inapungua kutokana na matokeo yatakavyokuwa ndio maana wakati ule kulikuwa na muunganiko na umoja wa hali ya juu sana kuanzia kwa wafanyakazi hadi kwa wachezaji na benchi lao la ufundi. Utaratibu huo ulisaidia kwa kiasi kikubwa watu wa nje ya uwanja kuisapoti timu na vijana hao wa mmiliki wa timu ndiyo walikuwa chachu ya kila kitu. Sasa hakuna nafasi ya wahudumu wa uwanja kwa mfano kupata posho inayotokana na matokeo ya timu ndani ya uwanja. Upande wangu naamini kwamba mtoto wa mfalme anapaswa kuishi katika mazingira yanayokidhi hadhi ya mtoto wa kifalme. Kilichowaondoa vijana hao wa mmiliki wa Azam FC katika timu ‘kususa’ ni maneno ambayo yalipelekwa kwa mzee wao kwamba wamekuwa wakitumia kiasi kikubwa cha pesa katika maisha yao ya kawaida. Wakatengenezewa ‘majungu’ na wageni hao na ili kuepusha lawama vijana hao wakaamua kujiweka kando na kuachana na mambo ya timu. Hilo limewaumiza na linaendelea kuwaumiza wengi pale Azam Complex kwa maana hivi sasa wengi wanategemea mishahara tu na si vinginevyo. Nakumbuka mwanzoni mwa mwaka 2014 niliandika jinsi wachezaji wa timu hiyo walivyokuwa wakipigia majungu kwa mmiliki wa timu na nikasema ili Azam FC ifanikiwe kupata ubingwa bosi wa timu hakupaswa kuzungumza na baadhi ya wachezaji waliokuwa wakimpigia simu na kuzungumzia mambo ya timu kwa siri. Baadhi ya wachezaji wa Azam wakati ule walikuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na mmiliki wa timu kiasi cha kufikia kutengenezea majungu na kuwachongea makocha kama Boris Bunjak. ‘Kujiondoa katika timu kwa watoto wa mmiliki Azam FC ni tatizo…?’

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni