Jumatano, 21 Septemba 2016

MANENO YA KASSIM DEWJI 'KD', HANA WASI HATA KIDOGO, ANA IMANI SIMBA WATAIMALIZA YANGA YA PLUIJM

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Simba, Kassim Dewji, ameibuka na kusema kuwa kwa jinsi kiwango cha timu yao kilivyo imara kwa sasa wana asilimia 99 ya kuifunga Yanga katika mchezo wa Oktoba Mosi kwenye Uwanja wa Taifa na kudai kuwa iwapo mahasimu wao hao watawafunga ni kwa mipango tu kuanzia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Simba na Yanga zinatarajia kukutana Oktoba Mosi katika Uwanja wa Taifa jijini Dar katika mchezo wa saba wa Ligi Kuu Bara ambao unatarajiwa kuwa na ushindani wa hali ya juu kutokana na uimara wa kila upande. Dewji alisema kuwa, kiwango kinachoonyeshwa na Simba msimu huu ni cha hali ya juu na kimerejesha morali ya mashabiki na kudai kuwa lazima wawafunge Yanga bila ya wasiwasi wowote. “Kwa Simba hii lazima tuifunge Yanga itake isitake kwani tuna kikosi kizuri imara na chenye ushindani wa hali ya juu kutokana na kila mchezaji kujituma uwanjani. “Mahasimu wetu Yanga wasubirie kipigo siku hiyo na kama kutufunga labda watufunge kwa mipango kuanzia TFF na kwingineko lakini kwa jinsi timu ilivyo kwa sasa si rahisi kutufunga tunatarajia ushindi siku hiyo kwa kuanza tumeanza na Azam. “Kwa ujumla usajili wa msimu huu umekwenda vizuri na wachezaji wote tuliowasajili ni wazuri na wanaonekana kucheza katika kiwango kinachotakiwa na lengo letu ni kuona tunafanikiwa kutwaa ubingwa,” alisema Dewji.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni