Alhamisi, 22 Septemba 2016

Oktoba 1 Bet Uliwe kule tambwe huku mavugo ukizubaa tu, unakanyagwa

Na Ayoub Hinjo Zimebaki siku chache ili tuweze kuona pambano la watani wa jadi katika msimu huu mpya wa 2016/17. Ni mechi ambayo inavuta hisia za mashabiki na watu wengine kwa ujumla ambao si wafuatiliaji wa mchezo huu wa mpira wa miguu. Kila timu inaonekana kujipanga kisawasawa msimu huu. Mtihani wa Simba ulianzia kwa Mtibwa ambao wamekuwa wanatoa changamoto sana kwa timu zingine lakini Simba walifanikiwa kushinda mchezo huo 2-0. Mtihani mwingine uliofuata ulikuwa dhidi ya Azam ambao walikuwa wako imara baada ya kuondoka jijini Mbeya na alama 6 lakini Simba alishinda kwa 1-0. Msimu wa jana Simba walifungwa michezo yote miwili. Michezo yote walipoteza kwa kufungwa 2-0. Je na msimu huu watakubali kuona ushindi ukienda Jangwani!? Tusubiri Oktoba Mosi. TAMBWE NA NGOMA Muweke kando Obrey Chirwa ambaye amenunuliwa msimu huu na Yanga ili kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji. Mwiba kwa timu za Tanzania ni Tambwe na Ngoma ambao wanaonekana kuelewana zaidi. Ubora na maelewano yao umekuwa shida zaidi kwa mabeki wa timu pinzani. Katika michezo miwili iliyopita walifanikiwa kuiangamiza Simba huku Tambwe akifunga magoli mawili na Ngoma akifunga moja. MWANJALI NA LUFUNGA Msimu ulioisha Simba walikuwa na tatizo la beki wa kati. Mabeki wao hawakuwa na nidhamu ya ukabaji hicho ndicho kilipeleka msiba mitaa ya Msimbazi kwenye michezo yote miwili waliyocheza na Yanga. Tangu msimu kuanza Mwanjali na Lufunga wamekuwa wakicheza pamoja. Wametengeneza mseto mzuri kwenye timu hiyo. Mwanjali ni beki ambaye amekuwa na nidhamu katika ukabaji wake dhidi ya Azam alikula sahani moja na John Bocco ambaye alishindwa kufurukuta kabisa. Kwenye mchezo dhidi ya Yanga beki huyo atakuwa na kazi ya kutembea na Tambwe ambaye ni mviziaji mahiri. Staili ya uchezaji ya Tambwe inafahamika lakini ukizubaa kidogo tu anakuliza. Lufunga mara nyingi amekuwa anasimama kama beki wa mwisho kuhakikisha usalama zaidi kwa mlinda mlango. Kasi ya Ngoma inaweza kuwa shida kwake sababu si mzuri sana katika kumzuia mtu mwenye kasi. Bado Simba wanaweza kumchezesha Juuko Murshid katika nafasi ya Lufunga ili kumdhibiti Mzimbabwe huyo. AJIBU, MAVUGO NA KICHUYA Tangu kuanza kwa msimu mpya Simba wamekuwa wakiringa na wachezaji wao watatu waliopo kwenye safu ya ushambuliaji ambao ni Ajibu, Mavugo na Kichuya. Mavugo na Kichuya watavaana na Yanga kwa mara ya kwanza wakiwa ndani ya uzi wa Simba. Mavugo anaonekana bado hajatulia sawia sababu amekuwa anakosa sana magoli ya wazi lakini ni mchezaji wa kuchungwa na mabeki wa Yanga. Kichuya ana kasi sana na amekuwa akitumia mbio zake kama silaha ya kuwapigia wapinzani. Mtindo wake wa uchezaji wa kuingia ndani anapokuwa na mpira unaongeza idadi ya wachezaji wa Simba katika eneo hilo la ushambuliaji pia ni mwepesi katika kufanya ukabaji pale timu yake inapokuwa haina mpira. Ajibu ni kiunganishi cha mashambulizi ya Simba. Ana uwezo mkubwa kutengeneza nafasi za magoli na pia kufunga ni mzuri pia. Ndiye mchezaji pekee ambaye ndio ufunguo wa mashambulizi ya Simba katika kuwafunga mabeki wa timu pinzani. BOSSOU NA ANDREW Yanga ina machaguo mengi katika safu ya ulinzi hasa nafasi ya mabeki wa kati. Bossou na Andrew wanaonekana kupewa nafasi zaidi msimu huu. Kocha ameamua kufanya mapinduzi katika safu hiyo ambayo ilikuwa inakaliwa na Yondani pamoja na Nadir. Bossou ni mtulivu sana anapokuwa na mpira pia ni beki ambaye ana uwezo wa kuanzisha mashambulizi kutokea nyuma. Upande wa Andrew au Dante ni beki ambaye yupo vizuri pia mipira ya juu na hata katika kufanya ukabaji amekuwa na nidhamu. VITA ENEO LA KATIKATI NA PEMBENI Yanga wana Rasta mmoja hivi anaitwa Kamusoko. Huyu ndio kila kitu katika timu hiyo. Kamusoko ndio moyo wa Yanga katika kushambulia na kuzuia pia. Vilevile ni muhimili wa Yanga katika maamuzi ya kuichezesha timu. Tatizo kubwa kwake ni kukosa mchezaji sahihi ambaye atamfanyia kazi ya kuzuia japo mara nyingi amekuwa akianza na Twite ambaye ni kiraka na mara kadhaa amekuwa akicheza na Niyonzima ambaye ni mzuri zaidi katika kushambulia kama ilivyo kwake. Simba msimu huu wapo na Mkude pamoja na Mzamiru ambao wameonekana kuwa na muunganiko mzuri katika kuifanya timu ishambulie na kuzuia. Wameelewana mapema na kizuri zaidi ni jinsi walivyojipangia majukumu wanapokuwa uwanjani ambayo yameonekana msaada zaidi kwa timu ya Simba. Upande wa pembeni ni mara chache sana kushuhudia Simba wakishambuliwa upande wa kushoto ambao una Mohammed Hussein ambaye msimu huu anaonekana yupo katika ubora wake pia ni mzuri katika kupandisha timu ambapo hadi sasa amepiga mipira minne iliyozaa magoli. Upande huo mara nyingi umekuwa ukitumiwa na Msuva ambaye ana kasi na maamuzi binafsi ya kuisaidia timu. Wasiwasi mkubwa kwa Simba ni upande wa kulia ambao hadi sasa hauna mwenyewe. Simba bado hawajaziba upande huo ambao ulikuwa unatumiwa na Hassan Kessy ambaye yupo Yanga sasa. Deus Kaseke amekuwa akitumika upande huo kama winga wa kushoto wa Yanga na amekuwa msumbufu kwelikweli kwa staili yake ya kuingia ndani na mpira. Upande wa mabeki wa Yanga Juma Abdul na Haji Mwinyi wanaonekana kuwa katika viwango vyao bora vya siku zote. VITA YA PLUIJM NA OMOG Si mara ya kwanza wanakutana. Waliwahi kukutana wakati Omog yupo Azam ambapo michezo yote miwili walienda sare ya 2-2 na 1-1. Sasa wanakutana tena lakini Omog yupo ndani ya Simba na ameijenga Simba kuwa timu tishio zaidi hadi sasa. Hans Pluijm anajivunia kipigo alichokitoa msimu ulioisha kwa Simba. Omog anaangaliwa zaidi kuelekea mchezo huo sababu timu yake ya Simba haijafanikiwa kupata ushindi dhidi ya Yanga kwa msimu wa jana. Matokeo dhidi ya Mtibwa na Azam yanafufua matumaini kwa Wanamsimbazi katika kuelekea mchezo huo ambao ni mgumu kuutabiri.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni