Jumatatu, 19 Septemba 2016

WAKIMATAIFA YANGA YAWEKA REKODI MPYA LIGI KUU TANZANIA BARA

Yanga inaonekana imepania kwelikweli baada ya kutinga kwenye nafasi ya pili ya msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na rekodi ya pekee ya kutoruhusu kufungwa bao lolote mpaka sasa baada ya kucheza mechi nne ambazo ni sawa na dakika 360. Awali, kabla ya michezo ya wikiendi iliyopita, Yanga na Kagera Sugar ndiyo timu pekee zilizokuwa hazijaruhusu wavu wake kutikiswa lakini sasa imebaki peke yake kati ya timu nyingine 15 zinazoshiriki ligi hiyo baada ya Kagera iliyo chini ya Mecky Maxime kupigwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar.  Yanga imethibitisha ubora wa ukuta wao baada ya kuhimili kutoruhusu nyavu zake kuguswa licha ya kubadili wachezaji wa nafasi ya ulinzi mara kwa mara lakini pia imehimili hali hiyo katika viwanja vinne tofauti mpaka sasa. Katika mechi ya kwanza, Yanga imecheza na African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar na kushinda mabao 3-0, huku safu yao ya ulinzi ikiongozwa Vincent Bossou, Andrew Vincent ‘Dante’, Hassan Kessy na Haji Mwinyi. Mchezo uliofuata waliumana na Ndanda FC huko Mtwara kwenye Uwanja wa Nangwanda, mechi hiyo iliisha 0-0 na ukuta wa Yanga siku hiyo ulikuwa chini ya nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Dante, Mwinyi na Juma Abdul. Baada ya hapo ikarejea Uwanja wa Uhuru, Dar na kuichapa Majimaji mabao 3-0 na kwenye safu ya ulinzi alisimama Abdul, Mwinyi, Cannavaro na Dante ambaye baadaye aliumia na kumpisha Kelvin Yondani. Juzi pia waliipigiza Mwadui FC mabao 2-0 wakiwa katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, safu ya ulinzi ilikuwa mikononi mwa Yondani, Dante, Mwinyi na Abdul ambaye ni mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara 2015/16. Katika ushambuliaji Yanga imefungana na Simba kwa kufunga mabao mengi zaidi ya timu nyingine, timu hizo zote zimefunga mabao nane kwa wastani wa kufunga mabao mawili katika kila mechi. SOURCE: CHAMPIONI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni