Tayari imewekwa wazi mapema kuwa baada ya kukamilika kwa Uwanja wa Uhuru, timu za Simba na Yanga zitahamia hapo kwa ajili ya mechi zao za nyumbani za Ligi Kuu Bara, suala hilo halijaifurahisha Simba na limepingwa vikali. Awali, kabla ya juzi wajenzi wa uwanja huo kuukabidhi rasmi kwa serikali, tayari Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura aliweka wazi kuhusiana na azma hiyo ya kuzihamishia mechi za timu hizo kutoka Uwanja wa Taifa na kuhamia Uwanja wa Uhuru. Kocha Msaidizi wa Simba, Mganda, Jackson Mayanja ametoa sababu za kuukataa uwanja huo kuwa utawanyima uhuru wachezaji kuzalisha kile walichojifunza wakiwa mazoezini na kuwabana katika ufanisi wao wa kazi. “Uwanja wenye nyasi bandia kama huo utawanyima wachezaji kuzalisha kile walichokusudia, kwa maana mazoezi na mbinu wanajifunza kwenye uwanja halisi lakini wakienda kwenye mechi wanakutana na kitu kingine, hii itawanyima uhuru wa kufanya ubunifu na mbinu walizonazo. “Nyasi halisi kama zile za taifa ni nzuri zaidi na zinaleta uhalisia wa soka, tofauti na hizi bandia. Nafikiri kama kuna uwezekano wa mtu mwenye uwezo wa kugharamia gharama za Uwanja wa Taifa, mamlaka iwape tu uwanja huo kwa ajili ya matumizi lakini vinginevyo Uwanja wa Uhuru hautakuwa mzuri kwa wachezaji,” alisema Mayanja. SOURCE: CHAMPIONI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni