Ijumaa, 26 Agosti 2016

MAFANIKIO YA SERENGETI BOYS YASIGEUKE KUWA NGAO YA KUFICHA MAOVU YA TFF

KWANZA nianze na kuipongeza kwa dhati kabisa timu ya vijana ya chini ya miaka 17, Serengeti Boys kwamba imepita mengi hadi kufikia ilipo. Kama itafanikiwa kuing’oa Congo katika dakika 180, yaani mechi mbili zijazo, itakwenda kucheza Kombe la Mataifa Afrika ambalo litakuwa jambo jema kwa Watanzania. Vijana wetu wanahitaji kujifunza zaidi na kupata nafasi ya kujitangaza. Kushiriki michuano hiyo mikubwa ya Afrika ni sehemu ya kujitangaza na kupata nafasi ya kujiendeleza zaidi. Niwaase, kwamba pamoja na pongezi ninazotoa mimi au Watanzania wengine, bado kuna mengi ya kufanya. Niwakumbushe hivi, kazi bado haijaisha kwa kuwa wanatakiwa kuwatoa Congo ambao wanaonyesha pia wana kikosi kizuri. Kuwatoa lazima kuwe na ugumu, lakini inawezekana kwa kuwa ninaamini Serengeti Boys ina kikosi bora, pia ina makocha wazuri wakiwemo mzalendo Bakari Shime na Mdenishi, Kim Poulsen. Niwapongeze pia TFF kwa juhudi wanazozionyesha katika timu hiyo. Pia ule uamuzi wa kutusikiliza sisi wadau kwamba walikurupuka kumuondoa Poulsen, kwa kuwa tu walitaka kusafisha watu wote wa Leodegar Tenga bila ya kujali ubora wa kazi wanazofanya. Mwisho wamemrudisha Poulsen na wote tunaona hatua zinazopigwa kwa kuwa kweli, kocha huyo alijitahidi sana kuwainua vijana na Simon Msuva pamoja na Frank Domayo ni sehemu ya mfano wa kuonyesha ubora wake. Pamoja na hivyo tukubali, kufeli kwa Serengeti ni kufeli kwetu sote kwa kuwa hiyo ni timu ya taifa letu na wala si taifa la TFF. Kwa wale ambao wamekuwa hawaiungi mkono, hawajachelewa na wala hawalaumiwi kwa kuwa walikuwa na haki ya kusita kwa vile mambo mengi ya soka hapa nyumbani, yamejaa ubabaishaji. Wanapaswa kuwa na hofu. Sasa waondoe hofu, tuungane pamoja na kuwapa vijana wetu sapoti ya kutosha na ikiwezekana serikali nayo iingie kuongeza nguvu zaidi ya vile ambavyo imesema. Dakika 180 zilizobaki na hasa 90 za nyumbani ni muhimu sana na Watanzania wanapaswa kuungana wakiongozwa na serikali ili timu ifanye vema. Ambacho kimenivuta kuandika makala haya, ni hayo niliyoyaeleza hapo juu. Kuipongeza timu, kuiasa na kuwakumbusha Watanzania wengine kwamba hawajachelewa kuingilia kuiunga mkono. Ninalo la mwisho, kwamba TFF inapaswa kujua kuwa mafanikio ya Serengeti Boys hayawezi kuwa ndiyo ngao ya kila maovu wanayofanya TFF. Eti sasa wako ‘busy’ na Serengeti Boys au wakiulizwa jambo jingine waliloboronga, wanauliza kwani Serengeti Boys hamuioni? Sidhani kama Watanzania wataruhusu TFF ifanye madudu rundo kwa kuwa imepata Serengeti Boys na kutaka kuigeuza kichaka cha kujificha baada ya kuboronga mambo kadhaa. Hii si sawa na TFF wanapaswa kujipanga. Mambo yote waliyoboronga wanatakiwa kuwa wahusika na wanaopaswa kuyarekebisha au kuyatolea ufafanuzi. Mfano suala la Stand United, kila mmoja anaona si sawa, isipokuwa wachache wenye tamaa ya fedha ama wasio na haya hata kidogo. TFF ipo kimya na inajua kinachoendelea. Inaona sawa huenda inafaidika au inafurahia. Hili haliwezi kufunikwa na Serengeti Boys inavyokwenda, halihusiani hata kidogo. Kuna hoja za kujibu kuhusiana na mambo mengi ambayo hayaendi vizuri katika soka. TFF inajua imefeli katika mengi sana na huenda kweli ilikuwa na hamu ya kuona kuna sehemu ya kusifiwa baada ya kuboronga karibu kila kitu na kushindwa kuonyesha mabadiliko hata kidogo kama ulivyojigamba uongozi wa Malinzi wakati unaingia madarakani. Nani anaweza kusema umebadilisha nini, kiko wapi? Sasa Serengeti ndiyo inaonekana ngao, vingine visahaulike? Haiwezekani. Tutaendelea kuiunga mkono Serengeti Boys kwa kuwa ni timu ya Watanzania, lakini lazima tuendelee kuhoji kila ambacho hakipo sawa. Msikubali kuzibwa midomo ya kuhoji mambo mengi eti kwa kuwa Serengeti Boys inafanya vizuri. SOURCE: CHAMPIONI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni