pata dondoo mbalimbali za michezo ya ndani na nje ya nchi.mompondazy itakujuza kila kitu.
Alhamisi, 25 Agosti 2016
VIWANJA VYA NYUMBANI VIMETENGENEZA NUSU FAINALI YA ZESCO V SUNDOWNS, AFRIKA, YANGA IJIFUNZE HAPA…
TIMU mbili kutoka Kusini mwa Afrika zimefuzu kucheza nusu fainali ya Caf Champions League na sasa ukanda huu utakuwa na nafasi nyingine ya kushuhudia mojawapo ya timu za Kusini mwa Afrika ikifika fainali ya michuano hiyo baada ya kipindi kirefu kupita.
Msimu uliopita, timu 3 kati ya 4 zilizofuzu kwa nusu fainali zilitoka Afrika Mashariki na Kati na kombe la michuano hiyo mikubwa zaidi barani Afrika upande wa klabu likachukuliwa na TP Mazembe ya DR Congo ambayo iliwashinda Wasudan, El Merreikh katika nusu fainali. Al Hilal ya Sudan pia ilifika nusu fainali ya michuano hiyo mwaka uliopita.
Zesco United v Mamelod Sundowns
Ni game ya nusu fainali ya Champions League msimu huu ambayo itazikutanisha timu kutoka Zambia (Zesco) na nyingine kutoka Afrika Kusini. Mechi ya kwanza inataraji kupigwa kati ya tarehe16 hadi 18 mwezi ujao, kisha wiki mbili baadae timu hizo zitarudiana nchini Afrika Kusini.
Zamalek SC v Wydad Casablanca ni mechi nyingine ya nusu fainali ambayo itawakutanisha mabingwa mara 5 wa michuano hiyo na waarabu hao wa Morocco.
VIWANJA VYA NYUMBANI VIMEWABEBA ZESCO, SONDOWNS
Baada ya Zesco kufuzu katika hatua ya makundi, mshambulizi wa timu hiyo raia wa Tanzania, Juma Ndanda Liuzio aliniambia kwamba, mkakati mkubwa wa timu yake ni kuhakikisha wanakusanya alama zote 9 katika game zao 3 za nyumbani. Hadi kufikia hatua hiyo ya makundi, Zesco haikuwa imepoteza game yoyote katika uwanja wao wa nyumbani.
Walishinda 4-1 nyumbani katika mchezo wa raundi ya kwanza dhidi ya Horoya AC ya Guinea kabla ya kupoteza 2-0 ugenini. Wakafuzu raundi ya pili kwa jumla ya magoli 4-3 (uwanja wa nyumbani uliwabeba.) Katika raundi hiyo ya pili walishinda 3-1 ugenini kisha 2-1 nyumbani na kuwaondoa Stade Mallien ya Mali kwa jumla ya magoli 5-2.
Upande wa Sundowns, nao hawajapoteza game yoyote katika ardhi ya nyumbani. Raundi ya kwanza walikutana na AC Leopards ya Congo-Brazzaville na kushinda 2-0 nyumbani, na kulazimisha sare ya 1-1 ugenini (uwanja wa nyumbani uliwabeba pia).
Raundi ya pili walipoteza 1-0 ugenini mbele ya AS Vita Club ya DR Congo, wakashinda 2-1 nyumbani. Matokeo hayo yaliwaondoa katika michuano Sundowns kwa sheria ya goli la ugenini lakini wakarejeshwa na Caf baada ya kugundulika Vita Club ilimtumia mchezaji asiyestahili.
Katika michezo yao miwili ya nyumbani katika group stage, Sundowns ilishinda yote dhidi ya Zamalek na Enyimba. Kumbuka kundi la pili likuwa na timu 3 tu kufuatia, ES Setif ya Algeria kuondolewa katika michuano baada ya mashabiki wao kufanya vurugu katika game ya kwanza waliyopoteza dhidi ya Mamelodi.
Wasauz hao wamemaliza kama vinara wa kundi wakiwa na alama 9 kufuatia kushinda game nyingine moja ya ugenini. Zamalek wamemaliza katika nafasi ya pili wakiwa na alama 6 na Enyimba wametupwa mkiani wakiwa na pointi 3 tu.
Zesco ilimaliza game yao ya tatu ya nyumbani kwa sare ya kufungana 1-1 na Wydad siku ya jana Jumatano na kuwafanya wakusanye alama 9, na kumaliza katika nafasi ya pili ya kundi A. Pointi 7 wamekusanya nyumbani na nyingine mbili wamefanikiwa kupata katika game 3 za ugenini.
SOKA LA KUSINI MWA AFRIKA LINAANZA KUINUKA UPYA?
El Merreikh, Al Hilal na TP Mazembe ni timu ambazo zimezoeleka katika michuano ya CAF lakini kitendo cha timu kama Zesco, Sundowns na hata Yanga SC kufika hatua ya makundi katika michuano ya CAF ni dalili nzuri kwa ukanda wa Kati na Kusini mwa Afrika.
Ni dalili za kunyanyuka kwa klabu mpya ambazo zinaweza kushindana na zile za Kaskazini na Magharibi mwa Afrika ambazo zimetawala sana soka la Afrika kwa miaka hii 16.
Kuona timu 6 tofauti za Kati na Kusini mwa Afrika zikicheza makundi ya Caf huku 5 zikifika nusu fainali (Al Hilal, Merreikh, TP, Zesco na Sundowns) ni jambo la kujivunia huku Mazembe wakifika fainali na kushinda ubingwa mwaka uliopita, sasa timu nyingine ya ukanda huu itakuwa na nafasi ya kurudia mafanikio hayo mwaka huu.
Mazembe wako nusu fainali katika Confederation na Zesco watawavaa ndugu zao wa Kusini, Sundowns katika nusu fainali ya ligi ya mabingwa. Zesco v Sundowns nusu fainali yenye kurejesha soka la Kusini, Caf, Yanga ijifunze hapa…
Kwa ukaribu zaidi, tafadhali unaweza ku-LIKE PAGE yangu #BSports Tanzania . Utapata Updates za michuano mbalimbali.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni