Beki mpya wa kulia wa Simba, Hamad Juma, jana asubuhi alianguka bafuni akiwa nyumbani kwake na kusababisha achanike kisogoni kwake. Juma alijiunga na Simba msimu huu wa Ligi Kuu Bara akisaini mkataba wa mwaka mmoja akitokea Coastal Union baada ya mkataba wake kumalizika. Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi Jumatatu limezipata jana jioni na kuthibitishwa na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, tukio hilo lilitokea nyumbani kwake kabla ya kukimbizwa Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam alipokwenda kulazwa. Manara alisema, beki huyo mara baada ya kufikishwa hospitalini hapo, madaktari walishauri alazwe kutokana na damu nyingi zilizokuwa zinamtoka. "Hamad ameanguka na amepoteza damu nyingi sana, alipata matatizo hayo akiwa nyumbani kwake wakati anaingia bafuni na hivi sasa ninavyoongea na wewe yupo Hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya matibabu. "Madaktari wamelazimika kumuongezea damu beki huyo kutokana na kutoka nyingi, lakini tunashukuru hivi sasa anaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu ya haraka na madaktari hao, amelazwa wodi namba tano," alisema Manara. Aidha alipotafutwa Daktari Mkuu wa timu hiyo, Yassin Gembe kuzungumzia hilo, alisema: "Ninaomba nipigie baadaye hivi sasa nipo hospitali na nipo 'busy' na mgonjwa, ninaomba umpigie Manara atakupa taarifa nzima.” SOURCE: CHAMPION
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni