Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, amemwambia Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm kuwa ana mifumo na mbinu nyingi za uchezaji, hivyo asijidanganye kwa mechi mbili alizowaona wakiwa uwanjani kwamba ndiyo wamemaliza kazi. Pluijm ameonekana Uwanja wa Taifa mara tatu akiifuatilia Simba. Alianza kwa kuitazama ilipocheza michezo ya kirafiki dhidi AFC Leopards ya Kenya (walishinda mabao 4-0), kabla ya kutoa sare ya 1-1 na URA na juzi alikishuhudia kikosi hicho wakati kikiichakaza Ndanda kwa mabao 3-1. Katika mechi hizo zote, kocha huyo alionekana kuwa makini uwanjani huku akiwa na kalamu pamoja na karatasi akiandika baadhi ya vitu. Akizungumza na Championi Jumatatu, Omog alisema wapinzani wake wasitegemee alivyocheza mechi na Ndanda FC na nyingine zilizopita, basi atacheza hivyo katika mechi zote huku akitamba kuwa ana mifumo mingi atakayoweza kuitumia ndani ya uwanja. Omog alisema mfumo na aina ya soka anayoitumia inategemea aina ya timu anayocheza nayo, hivyo kabla ya mechi lazima awasome wapinzani wake ili ajue mbinu wanazozitumia. Aliongeza kuwa, katika mechi zote alizocheza hadi hivi sasa, ametumia mifumo miwili pekee ambayo ni 4-4-2 na 4-5-1. “Mifumo na mbinu ninazozitumia ndani ya uwanja, zinategemea na aina ya timu ninayokutana nayo, hiyo ni baada ya kuwasoma wapinzani wangu. "Kila mechi nimekuwa nikibadili mifumo mbalimbali kwa lengo la kupata ushindi, hivyo hao wapinzani wangu wasitegemee kuwa hivi nilivyocheza na Ndanda ndiyo tutacheza, mimi ninabadilika kila siku,” alisema Omog. SOURCE: CHAMPIONI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni