Straika mpya wa Simba, Mrundi, Laudit Mavugo, amewaomba mashabiki wa timu hiyo wasimhukumu kwa lolote lililotokea Uwanja wa Taifa juzi walipoifunga Ndanda 3-1 huku akisisitiza kuwa ndiyo kwanza ameanza kazi. Hata hivyo, straika huyo amewaomba radhi mashabiki wa klabu hiyo kutokana na kuonekana kuwa mchoyo uwanjani katika nafasi ambazo wenzake wangeweza kufunga. Mavugo ambaye alifunga bao la kwanza katika ushindi huo katika mchezo huo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, amesema: “Nawaomba wapenzi na mashabiki wasiwe na hofu yoyote dhidi yangu kutokana na kutoonyesha kiwango kizuri katika mchezo huo kwa sababu kulikuwa na mambo najifunza lakini ni matumaini yangu kuwa mechi zijazo nitakuwa bora zaidi ya nilivyocheza. “Nawaomba watulie na wasiwe na wasiwasi na mimi nitawafanyia kazi na nitahakikisha ninafunga kila mechi endapo Mungu atapenda kwa sababu tayari nimeshaiona ligi ya Tanzania ikoje na ninatakiwa nichezeje.” Mavugo amejiunga na Simba hivi karibuni akitokea Vital’O ya Burundi na hadi sasa ameshaifungia mabao mawili katika mechi tatu moja ya ligi na mbili za kirafiki. SOURCE: CHAMPIONI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni