Jumatatu, 22 Agosti 2016

KESSY AANZA MAJUKUMU YA KIMATAIFA, AWAPANIA TP MAZEMBE

Beki wa pembeni wa Yanga, Hassan Kessy, amesema miongoni mwa mechi alizokuwa anatamani kucheza basi ni hii dhidi ya TP Mazembe itakayochezwa kesho Jumanne na ameahidi kupiga soka la nguvu. Yanga ambao wameondoka jana asubuhi kuelekea DR Congo, kesho Jumanne wanatarajiwa kuvaana na Mazembe kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Beki huyo alizikosa mechi za awali za Kombe la Shirikisho Afrika kutokana na utata kwenye usajili wake kutoka Simba kwenda Yanga lakini baada ya kuruhusiwa kuichezea Yanga wikiendi iliyopita, ameonekana kuwa mwenye furaha. Akizungumza na Championi Jumatatu, Kessy alisema alikuwa ana shauku kubwa ya kuichezea Yanga katika michuano ya kimataifa, hivyo baada ya TFF kumruhusu, basi mechi hiyo ataitumia kujitangaza kimataifa ili afungue milango ya kucheza soka nje ya nchi. Aliongeza kuwa, licha ya mwaka huu kuzikosa baadhi za mechi za kimataifa, amepania kuonyesha kiwango kikubwa wakati timu yao itakapovaana na Mazembe. “Mimi kitu cha kwanza kabisa kilichonileta Yanga ni michuano ya kimataifa, baada ya timu yangu hii mpya kushiriki, nikiamini hapa ndiyo sehemu sahihi kwangu kutimiza malengo yangu ya kucheza soka nje ya nchi. Hivyo basi nimepanga kuonyesha kiwango kikubwa kwenye mechi hii yangu ya kwanza kimataifa na Mazembe.  "Ninajua mechi hii haina umuhimu kwetu kwani tayari baada ya kupoteza michezo ya mwanzoni tumetolewa, lakini kikubwa heshima, hivyo ni lazima tupambane ili tupate ushindi wa ugenini," alisema Kessy. SOURCE: CHAMPIONI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni