Shirikisho la Soka la Kimataifa la Soka (FIFA), kwa mara nyingine limeipa nafasi Tanzania kwa kutoa kozi maalumu ya stamina (Physical fitness) kwa makocha wa Tanzania wenye leseni kiwango B inayoanza leo Agosti 22, 2016. Kozi hiyo inayoendeshwa na mkufunzi kutoka FIFA, Dk. Praddit Dutta, raia wa India itafikia ukomo Ijumaa wiki hii. Akifungua kozi hiyo, Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine aliishukuru FIFA kwa namna inavyoipa nafasi Tanzania katika kozi mbalimbali hususani za ukocha na uamuzi. “Si kila nchi inapata privilege (fursa) kama hii. Bila shaka FIFA inatambua uwezo wa makocha wa Tanzania kwa sasa. Mjue kuwa FIFA ina watu wa kuwapa taarifa kila kona “Kama mngekuwa mnafanya vibaya, FIFA wangesema Tanzania bado, kwa hiyo kozi zisipelekwe… lakini inaonekana mnafanya vema, mngefanya vibaya msingefikiriwa,” alisema Mwesigwa aliyekuwa mgeni rasmi katika ufunguzi huo. Mwesigwa amesema kwa kuwa FIFA ina malengo chanya na Tanzania kwa kutoa kozi mbalimbali ikiwamo hiyo ya physical fitness inayolenga kuwapa ujuzi makocha hao kuwajengea uwezo wachezaji kuwa na stamina. Hivyo akawataka makocha wanaohudhuria kozi hiyo kutumia fursa hiyo ya mafunzo si kwa ajili yao peke yao bali kuendeleza ujuzi huo kwa wengine ambao hawakubahatika kuwa sehemu ya wateule wa FIFA. Naye, Mkufunzi wa kozi hiyo, Dk. Dutta alisema: “Bila shaka Tanzania inakwenda kufungua ukurasa mwingine wa soka la weledi kwa kuwa na wataalamu mbalimbali katika ukocha na uamuzi. Mnachotakiwa ni kujitahidi kufanya vema na kozi nyingine nyingi zinakuja.” FIFA kwa kushirikiana na Idara ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), chini ya Mkurugenzi Salum Madadi, imepitisha majina ya makocha 27 kuhudhuria kozi hiyo inayofanyika katika Hosteli ya TFF iliyoko kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam. Makocha wanashiriki kozi hiyo ni Mohammed Muza, Samwel Moja, Nassa Mohammed, Jemedari Said, Oscar Mirambo, Wane Mkisi, Cletus Mutauyawa, Shaweji Nawanda, Kizito Mbano, Dennis Kitambi, Sebastian Nkoma, Fikiri Mahiza, Nyamtimba Muga, Nassor Mwinchui, Alfred Itaeli, Henry Ngondo, John Tamba, Kidao Wilfred, Luhaga Makunja, Mohammed Tajdin, Mohammed Silima, Salum Ali Haji, James Joseph, Kessy Mziray, Daudi Sichinga, Bakari Shime na Salum Mayanga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni