Beki mpya wa kulia wa Simba, Hamad Juma, juzi asubuhi alianguka bafuni akiwa nyumbani kwake na kusababisha achanike kisogoni kwake. Mara baada ya kutoka kwa taarifa hiyo ambayo siyo nzuri kwa Wanasimba, hofu ilitawala miongoni mwao lakini habari ni kuwa mchezaji huyo anaendelea vizuri na ameshapatiwa matibabu na kuruhusiwa kutoka hospitali. Juma ambaye alijiunga na Simba kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Coastal Union, mwanzoni mwa msimu huu alikutwa na majanga hayo nyumbani kwake kabla ya kukimbizwa Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam alipokwenda kulazwa. Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara alisema beki huyo mara baada ya kufikishwa hospitalini hapo, madaktari walishauri alazwe kutokana na damu nyingi zilizokuwa zinamtoka lakini sasa anaendelea vizuri. Awali Manara alinukuliwa akisema kuwa mchezaji huyo alianguka wakati alipokuwa akiingia bafuni ambapo madaktari walilazimika kumuongezea damu baada ya kupoteza damu nyingi kutokana na jeraha hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni