Azam FC imeamua kuliandikia barua Shirikisho la Mpira wa miguu nchini (TFF) wakitaka michezo yao dhidi ya Simba na Yanga ipigwe kwenye uwanja wao wa Azam Complex na siyo kucheza kwenye uwanja wa taifa ambako mara zote wamekuwa wakicheza pindi wanapokutana na vilabu hivyo vikongwe nchini. “Tumepeleka barua yetu ya maombi au malalamiko kwa TFF ili mechi zetu za nyumabni ambazo tunacheza na klabu za Simba na Yanga waje kwenye uwanja wetu wa Azam Complex badala ya kwenda kucheza kwenye uwanja wa taifa” amethibitisha Jafar Idd ambaye ni msemaji wa Azam FC. “Kwa historia, timu hizi zimewahi kuutumia uwanja wa Azam Complex kama uwanja wao wa nyumbani na kucheza mechi zaidi ya nne wakati uwanja wa taifa ulipokuwa unamatatizo kwahiyo tunaona hakuna sababu ya kutoutumia uwanja huo wetu dhidi ya vilabu hivyo pale tunapocheza kama wenyeji.” “Ili ligi iwe ya haki na usawa, kila mtu atumie uwanja wake wa nyumbani, club license ambayo kwa sasa ndiyo imekuwa gumzo inasema, jambo la kwanza kwa klabu ambayo itashiriki ligi kuu ya nchi lazima iwe na uwanja wake.” “Tumeomba kwa TFF mchezo wetu unaokuja dhidi ya Simba, basi taratibu hizo zifanywe ili tuweze kuutumia uwanja wetu wa nyumabani kwasababu sisi ndiyo tutakuwa wenyeji. Vinginevyo tutakwenda kutumia uwanja wa taifa pale timu hizo mbili zitakapokuwa wenyeji.” Azam imekuwa ikilazimika kucheza kwenye uwanja wa taifa mechi zake zote zinazohusisha vilabu vya Simba na Yanga, licha ya klabu hiyo kuwa na uwanja wake ambao umekidhi viwango vya kimataifa. Sababu kubwa zinazotolewa kwanini Azam haiutumii uwanja wake wa Azam Complex inapokutana na Simba na Yanga, ni ile ya wingi wa mashabiki wa klabu hizo ukilinganisha na uwezo wa uwanja.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni