Jumatano, 11 Januari 2017

ONYANGO AUMIA NA KUIACHIA MAJANGA UGANDA, YAPIGWA 3-0 KIPA namba moja wa Uganda, Denis Onyango aliumia jana wakati timu yake ikifungwa mabao 3-0 na na mabingwa wa Afrika, Ivory Coast katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Chuo Kikuu cha New York mjini Abu Dhabi. Pamoja na hayo, Onyango anatarajiwa kuwa fiti kabla ya mchezo wa kwanza wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Ghana Januari 17 Uwanja wa Port Gentil, Gabon. Kipa huyo wa Mamelodi Sundowns alianguka dakika ya 38 baada ya kuumia nyonga ya mguu wa kushoto. Hata hivyo, akapatiwa matibabu na kurudi kumalizia dakika 45 za kipindi cha kwanza timu zikirudi vyumba vya kubadilishia nguo zikiwa hazijafungana, lakini mwanzoni mwa kipindi cha pili msaidizi wake, Robert Odongkara akachukua nafasi. Denis Onyango aliumia jana na kuiacha Uganda ikifungwa mabao 3-0 na Ivory Coast katika mchezo wa kirafiki Abu Dhabi Na Ivory Coast wakafanikiwa kupata mabao matatu kupitia kwa Jonathan Kodjia dakika ya 51, Wilfried Zaha dakika ya 58 na Serge Aurier dakika ya 72. Akizungumza katika mahojiano maalum baada ya mchezo huo, Onyango alisema, “Ninatumaini kwamba nitakuwa fiti kabisa wakati wa mchezo na Ghana,". Kwa sasa yupo chini ya uangalizi wa dawati la tiba la The Cranes linaloongozwa na Dk Ronald Kisolo na mchua misuli, Ivan Ssewanyana ambao wataendelea kumtazama kwa siku nne. Onyango aliungana na kambi ya The Cranes Jumamosi mjini Dubai akitokea Abuja, Nigeria ambako alikwenda kuchukua tuzo yake Mwanasoka Bopra Anayecheza Afrika ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) 2016. Anatarajiwa kuisaidia sana Uganda kufanya vizuri kwenye fainali hizi za Afcon 2017 ambazo ni za kwanza kwa Cranes tangu mwaka 1978 walipofungwa na Ghana 2-0 kwenye fainali mjini Accra. Uganda itamenyana na Misri Januari 21 Uwanja wa Port Gentil kabla ya kukipiga na Mali kwenye mchezo wake wa kwanza wa Kundi D Januari 25.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni