Jumatatu, 16 Januari 2017

Hatujawahi kuihofia timu yoyote, tutapata ushindi vs Simba’ – Barnabas Kiungo-mshambulizi wa Mtibwa Sugar, Vicent Barnabas ametamba hawatishiki na kiwango cha Simba SC msimu huu. Timu hizo mbili zinakutana siku ya Jumatano hii zikiwa katika nafasi tofauti katika msimamo wa ligi kuu. Simba wanaongoza wakiwa na alama 44 baada ya kucheza michezo 18 na Mtibwa wapo nafasi ya nne wakiwa na pointi 30 baada ya kushuka dimbani mara 18 pia. Katika miaka sita ya hivi karibuni, Mtibwa imepoteza mchezo mmoja tu dhidi ya Simba katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro-walifungwa 1-0 msimu uliopita huku wakipoteza michezo miwili mfululizo ya ligi dhidi ya wababe hao wa zamani katika soka la Bara. Walifungwa 2-0 katika mchezo wa kwanza msimu huu na 1-0 katika mchezo wa pili msimu uliopita. “Hatujawahi kutishika dhidi ya timu yoyote ile, nadhani wao –Simba wanajua Mtibwa ni timu ya aina gani na ili ujue ubora wako ni lazima ucheze na aliye bora na upate matokeo,” anasema Barnabas akiwa Turiani, Morogoro siku ya leo Jumatatu. “Naamini tutapata matokeo mazuri. Tulipoteza mchezo wa kwanza katika uwanja wa Uhuru kwa sababu moja kubwa, wakati ule tunakuta wachezaji wetu wengi muhimu waliokuwepo msimu uliopita walihama. Timu ilikuwa ikijijenga upya na kama umeiona timu yetu hivi sasa hauwezi kusema tunashindwa. Naimani tutapata matokeo.” Anasisitiza mchezaji huyo wa zamani wa Taifa Stars na vilabu vya Kagera Sugar na Yanga SC. Salum Mayanga ambaye aliisimamia Mtibwa kama kocha mkuu katika michezo iliyopita ameteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ lakini kuondoka kwake hakujapunguza morari ya timu hiyo ikiwa chini ya Zubery Katwila na Patrick Mwangata. “Morai ipo juu, na kama unavyojua makocha wetu wa sasa Zubery Katwila na Patrick Mwangata wapo hapa kwa muda mrefu sana. Ni sehemu ya familia yao kwa miaka mingi hivyo wanajua Mtibwa inahitaji nini kwa sasa. Mechi itakuwa nzuri na mashabiki waje kwa wingi kutazama burudani.”

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni