Jumamosi, 28 Januari 2017

Homa ya Sadio Mane Liverpool si kitu kabisa inapocheza bila huduma ya staa huyo wa Senegal. Kukosekana kwa Mane klabuni Liverpool ni majanga makubwa, homa kali. HOMA ya maradhi mpya imeibuka huko Anfield inayoitwa ‘Ukosefu wa Mane!’ Mane? Ndiyo, ni yule staa wao Liverpool na timu ya taifa ya Senegal, Sadio Mane. Liverpool si kitu kabisa inapocheza bila huduma ya staa huyo wa Senegal. Kukosekana kwa Mane klabuni Liverpool ni majanga makubwa, homa kali. Ukitaka kujua hilo, tazama takwimu hizi. Liverpool kwa sasa inakosa huduma ya mchezaji huyo, ambaye amerudi Afrika kucheza michuano ya Afcon 2017 huko Gabon. Na tangu akosekane, imekuwa ni kupatwa kwa Liverpool. Wametupwa nje kwenye Kombe la Ligi na wakifungwa pia nyumbani Anfield na vimeo, Swansea City. Ipo hivi, kabla ya Mane kwenda Afcon, akiichezea Liverpool timu hiyo imeshinda mechi 17 kati ya 24 ilizocheza, lakini tangu aondoke, kwenye mechi sita ilizocheza Liverpool wameshinda moja tu. Kipindi ambacho Mane yupo, Liverpool ilikuwa na uhakika wa kushinda mechi zake kwa asilimia 71, lakini baada ya kuondoka, hali imeshuka na kuwa asilimia 17 tu. Wakati Mane akiwa kwenye kikosi, Liverpool ina uhakika wa kufunga mabao zaidi ya mawili, lakini bila ya huduma yake, wastani unaonyesha ni bao moja tu. Mane ametupia wavuni asilimia 33 ya nafasi zote alizopata kwenye Ligi Kuu England msimu huu, wakati fowadi mwingine Roberto Firmino ana asilimia 16 tu ya kutumbukiza wavuni nafasi alizopata kwenye ligi hiyo msimu huu. Hii ina maana Liverpool inakuwa hatari sana kwenye fowadi yake inapokuwa na huduma ya Mane.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni