Jumatatu, 16 Januari 2017

Juma Liuzio: ‘Sitashangilia nikiifunga Mtibwa Jumatano, ni mechi ngumu ila tutashinda…’Mshambulizi Juma Ndanda Liuzio aliye Simba SC kwa mkopo akitokea Zesco United ya Zambia anaamini mechi ya Jumatano hii vs Mtibwa Sugar itakuwangumu kwa kila upande hasa akichukulia ugumu wa kikosi hicho cha Turiani kinapocheza katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro dhidi ya timu kubwa nchini (Simba na Yanga SC). Liuzio alicheza kwa misimu mitatu Mtibwa kabla ya kuuzwa Zesco United miaka miwili na nusu iliyopita ataikabili timu yake hiyo ya zamani ambayo ilimlea na kumkuza kimpira kwa mara ya kwanza katika mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara. “Mechi yetu dhidi ya Mtibwa itakuwa ngumu sana kwa sababu Mtibwa huwa wagumu sana wanapokuwa nyumbani. Upande wangu nimejiandaa vizuri kimwili na kiakili. Sina presha yoyote na nitapambana kuisaidia timu yangu kupata ushindi,” anasema Liuzio nilipofanyanae mahojiano Jumatatu hii. Wachezaji wengi wa kulipwa husita kushangilia pindi wanapofunga dhidi ya timu zao za zamani-hasa zile zilizowasaidia kufika walipo, nilimuuliza Liuzio kama atashangilia ikitokea akafunga katika mchezowa Jumatano hii. “Kwa kweli sitashangilia nikifunga katika mchezo dhidi ya Mtibwa. Nitafanya hivyo kutokana na kuiheshimu timu hiyo iliyogundua kipaji changu na kukiendeleza. Walinitunza vizuri na hadi kufika hapa nilipo ni kwa sababu nilipitia Mtibwa. Nawaheshimu sana.” Liuzio alicheza michezo sita ya Simba katika michuano ya Mapinduzi Cup 2017 na kufunga goli moja. “Michuano ya Mapinduzi imenisaidia sana, kwanza nimefahamu Simba wanavyocheza pia wachezaji wenzangu tayari nimewafahamu vizuri. Niko tayari kucheza katika mfumo wowote na napenda kuwaambia mashabiki wa Simba wajitokeze kwa wingi siku ya mchezo kutusapoti kadri ya uwezo wao na sisi tutajituma kwa uwezo wetu kuhakikisha tunapata ushindi.”

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni