Jumatano, 30 Novemba 2016

Wacha nifunguke Uamuzi wa kutumia busara badala ya sheria na kanuni TFF mnautoa wapi? Huu utaratibu wa kutumia busara katika kufanya maamuzi ya kisheria na kanuni tumeutoa wapi? Taratibu zinajulikana, sheria zipo, kamati husika ipo, kilichokuwa kinatakiwa ni kulishughulikia jambo hili kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni kwa kuzingatia ushahidi wa pande zote mbili ili upande wenye haki upewe haki yake. Kuna faida mbili kama kamati ingesimama katika sheria kuliko kuipeleka kesi hii kishkaji na siasa za Simba na Yanga. Faida ya kwanza kama kesi hii ingeamuliwa kisheria ni kuijengea heshima na imani TFF na mamlaka husika kwa kusimama kwenye haki pasipo kuyumba na kutoa fundisho au angalizo kwa wengine kwamba taasisi haiyumbishwi imesimama kwenye mstari. Jambo la pili ni kutengeneza mazingira ya kuwasaidia wachezaji wenyewe kwamba hata kama wanafanya ujinga wa kufanya udanganyifu na kusaini timu mbili au kusaini timu nyingine wakati bado mikataba yao na timu nyingine ipo hai watakua wakijua lazima watakabiliwa na adhabu bila kujali ni wachezaji wa Simba au Yanga. Lakini inapofika wakati TFF inatoa nafasi kwa vilabu kumalizana nje ya sheria wanakuwa hawatatui tatizo la muda mrefu, vipi mambo hayo yakifanywa na vilabu kama Ruvu Shooting na Mbao FC? Msimu ujao huenda Simba wakamsajili mchezaji wa Yanga kimagumashi TFF haitakuwa na meno ya kuiadhibu Simba moja kwa moja kwasababu Yanga walipofanya hivyo TFF ilitoa nafasi kwa vilabu kumalizana kisela. Jana afisa habari wa TFF Alfred Lucas aliutangazia umma wa watanzania kwamba, kesi hiyo imerudishwa kwenye kamati ya sheria na hadhi za wachezaji kwa ajili ya kufanyiwa uamuzi, TFF imeiagiza Simba kupeleka mkataba halali waliosainiana kati ya Simba na Hassan Ramadhani Kessy pamoja na ushahidi unaothibisha kwamba Simba walikuwa wanamlipa Kessy hususan katika miezi mitatu ya mwisho. Sasahivi kesi imegeuka, mwanzo Simba walilalamika kuwa Kessy alivunja mkataba kwa kuanza kuitumikia Yanga wakati bado alikuwa na mkataba halali na klabu ya Simba. TFF badala ya kuamua Kessy ya msingi sasahivi inataka kujiridhisha kama Kessy alikuwa akilipwa mshahara au la! Mbona Kessy hakufungua kesi ya kuidai Simba? Kwahiyo, kama mchezaji akiwa anaidai klabu mishahara inabidi asajiliwe na klabu nyingine bila kufuata taratibu? Kwa mujibu wa taarifa za Simba, Kessy alibakiza siku chache ili mkataba wake na Simba umalizike, lakini hiyo haimaanishi mchezaji alitakiwa avae jezi za Yanga, kusafiri au kuhusika moja kwa moja na shughuli za Yanga ilibidi asubiri hadi mkataba wake umalizike. Baada ya Yanga kuona wamefanya kosa huenda Kessy aliwaambia makataba wake na Simba umemalizika lakini wao hawakujiridhisha, wanatafuta sehemu ya kusawazisha ndiyo maana wanaomba ushahidi (salary slip au bank statement) wa malipo ya mishahara ya Simba kumlipa Kessy. Sasa kama Simba walikuwa wanamlipa Kessy kishkaji kwa kutoa pesa mfukoni bila maandishi watashindwa kwenye kesi hii kwasababu wakishindwa kuthibitsha kwamba walikuwa wanamlipa Kessy kwa zaidi ya miezi mitatu, basi moja kwa moja mkataba utakuwa ulivunjwa na Simba wenyewe. Ngoja tuendelee kujionea sarakasi za Simba na Yanga kwenye soka la Tanzania huku jaji wao akiwa ni kipofu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni