Jumatatu, 28 Novemba 2016

BAADA YA KUMALIZANA NA SIMBA, ZIMBWE AWEKA WAZI KWAMBA DENI LIKO KWAKE, ANATAKA UBINGWA SIMBA Baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili, beki wa pembeni wa Simba, Mohamed Zimbwe maarufu kama 'Tshabalala', ametamka kuwa haidai timu hiyo lakini yenyewe ndiyo inamdai deni kubwa la kuhakikisha anaipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu. Tshabalala alisaini mkataba huo wiki iliyopita baada ya ule wa kwanza kubakiza miezi sita. Beki huyo anayecheza namba tatu, kabla ya kusaini mkataba huo alikuwa akiwaniwa vikali na Yanga ambayo ilitenga kitita cha Sh mil 60 ili kumnasa. Hata hivyo, Simba inafanya siri kuhusu dau ililompa ili amwage wino. Tshabalala alisema amepanga kuitumikia timu hiyo kwa mafanikio makubwa katika kipindi chote atakachokuwepo Simba. Tshabalala alisema, moja ya mafanikio atakayoanza nayo ni kuuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara nchini ya Kocha Mkuu Mcameroon, Joseph Omog. Aliongeza kuwa, Wanasimba watarajie mengi kutoka kwake, hiyo ni baada ya kumalizana na viongozi wake kwa kutimiza mahitaji yake muhimu aliyokuwa anayahitaji ikiwemo fedha ya usajili na mshahara mzuri, hivyo ni lazima afanye kazi katika kiwango cha juu ili kuipa mafanikio timu hiyo kwa kuwa sasa akili yake imetulia. “Mimi Simba siwadai, wao ndiyo wananidai, hivyo ni lazima nifanye kazi yangu vizuri katika kuhakikisha ninaipa mafanikio makubwa timu yangu ya Simba. "Mafanikio hayo ni kuipa mataji mbalimbali ya ubingwa kwa kuanzia huu wa ligi kuu, hivyo ninaahidi kupambana ndani ya uwanja kuhakisha ninafikia malengo yangu. “Na hilo litawezekana kama wachezaji, viongozi na benchi la ufundi tutaungana na kufanya kazi kwa pamoja kwa kushirikiana kwa kila mmoja kutimiza majukumu yake,” alisema Tshabalala.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni