Jumanne, 29 Novemba 2016

BAADA YA MZUNGUKO WA KWANZA, MAHADHI AWEKA WAZI KUCHOSHWA NA BENCHI LA YANGA Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Juma Mahadhi, amefunguka kwamba amechoshwa na maisha ya kukaa benchi katika kikosi hicho na katika mzunguko huu wa pili anajifua vilivyo kuhakikisha anaingia katika kikosi cha kwanza. Mahadhi aliyejiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu huu akitokea Coastal Union ya Tanga, amekumbana na ushindani mkubwa mbele ya viungo wenzake Simon Msuva na Geofrey Mwashiuya jambo ambalo linasababisha atumike kama chaguo la mwisho mbele ya nyota hao. Akionyesha kujiamini, Mahadhi amesema ameamua kuja kitofauti kwa ajili ya kujihakikishia namba ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha Mzambia, George Lwandamina ambapo atajitahidi kuongeza juhudi ili kupata nafasi hiyo. “Sasa hali ya kutocheza mara kwa mara imenichosha kwani nahitaji nafasi ya kuonyesha mchango wangu kwenye timu ambapo nimepanga katika mzunguko huu wa pili nijifue zaidi kwa ajili ya kuliaminisha benchi la ufundi na wanipe nafasi hiyo. “Najua kwamba haitakuwa kazi rahisi kwani ninaoshindana nao ni watu wenye viwango vikubwa kama mimi lakini hilo halitanifanya nikate tamaa kwani lengo langu ni kuona nacheza mara kwa mara,” alisema Mahadhi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni