Jumatatu, 28 Novemba 2016

AZAM FC YAVUNA VIJANA 10 U-17 MWANZA KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, jana imekamilisha zoezi la kusaka vipaji kwa vijana wenye umri wa miaka 17 (U-17) jijini Mwanza na kuvuna wachezaji 10. Majaribio hayo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini humo kuanzia saa 1.00 asubuhi, wakijitokeza jumla ya vijana 266 kabla ya kuorodheshwa 26 na mwishoni kupatikana 10 walio bora. Kiujumla zoezi hilo lilienda vema na benchi la ufundi la vijana chini ya Mkuu wa Maendeleo ya Soka la Vijana Azam FC, Tom Legg, limeridhishwa kwa kiasi kikubwa na majaribio hayo kutokana na vijana wengi wenye vipaji vya hali ya juu kujitokeza. Mpaka sasa zoezi hilo limeshahusisha mikoa mingine mitano, ambayo ni Dar es Salaam, Tanga, Morogoro & Dodoma, Mbeya na Visiwani Zanzibar. Katika maeneo yote hayo ikiwemo Mwanza, kwa mujibu wa takwimu jumla ya vijana 3, 265 wamefanyiwa usaili, kati ya hao 70 pekee ndio waliochaguliwa na 151 kuorodheshwa kwenye kumbukumbu za mradi huo kwa ajili ya matumizi ya baadaye. Kwa majaribio mengine ya wazi katika maeneo mengine kuzunguka Tanzania yatatangazwa hivi karibuni. #AzamFCU17Project

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni