Jumanne, 29 Novemba 2016

VIONGOZI SIMBA WAONA HII SASA NI KERO, WAAMUA KUACHANA NA MKUDE Katika siku za hivi karibuni kiungo mkabaji wa Simba, Jonas Mkude ambaye mkataba wake na timu hiyo unafikia tamati mwezi Januari mwakani, alisema kuwa mpaka sasa haelewi chochote kama ataendelea kuitumikia timu hiyo au la. Kutokana na hali hiyo, Mkude akawataka Yanga wakamsajili kama kweli wanamhitaji akidai bila kusita atasaini timu hiyo, kwani yupo tayari kuitumikia. Jambo hilo linadaiwa kuukera uongozi wa Simba na umeamua kuchukua jukumu la kukaa kimya bila ya kumfuatilia tena kiungo huyo na wamesema kama anataka kwenda Yanga aende. “Mkude hivi sasa anatakiwa kuwa makini sana, vinginevyo anaweza kujikuta katika wakati mgumu kwani uongozi umesema kuwa hautahangaika naye tena, yeye kama anataka kuondoka basi aondoke zake. “Wamefikia hatua hiyo baada ya kumbembeleza sana kusaini mkataba mpya lakini yeye amekuwa akizingua akidai kuwa fedha anazotaka kupewa ni kidogo lakini pia kila akiitwa kwa ajili ya mazungumzo amekuwa akikataa,” kilisema chanzo chetu cha habari na kuongeza: “Kutokana na hali hiyo uongozi wa timu unamsubiria kocha aje ili uweze kuzungumza naye na ikiwezekana aanze kuwa anamtumia Mzamiru Yassin kama kiungo mkabaji halafu Juma Awadh awe anacheza namba nane.” Alipotafutwa Mkude ili aweze kuzungumzia hali hiyo alisema: “Kama wamefikia uamuzi huo ni wao lakini binafsi kwa sasa siwezi kusema chochote juu ya suala hilo.”

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni