pata dondoo mbalimbali za michezo ya ndani na nje ya nchi.mompondazy itakujuza kila kitu.
Jumatano, 30 Novemba 2016
Kagera Sugar imemnasa Juma Kaseja Uongozi wa klabu ya Kagera Sugar umethibitisha kumnasa Juma Kaseja golikipa wa zamani wa Simba, Yanga na timu ya taifa Taifa Stars. Manager wa Kagera Sugar Mohamed Hussein amesema tayari wameshamnasa Kaseja huku bado wakiwa kwenye mazungumzo na baadhi ya wachezaji wengine kwa ajili ya kuimarisha kikosi chao kwa mujibu wa mapendekezo ya kocha wa timu hiyo. “Mwalimu alikuwa anahitaji kuongeza nafasi tatu, golikipa, beki wa kati pamoja na kiungo. Tayari tumesha mpata beki wa kati ambaye ni Mohamed Faki aliyewahi kucheza Simba na JKT Ruvu kwa upande wa golikipa tutamchukua Juma Kaseja kwa ajili ya kuziba nafasi ya golikipa,” amethibitisha Mohamed Hussein huku akisema tayari Kagera Sugar wapo kambini wakiendelea na mazoezi.
Maneno ya mwisho ya golikipa wa timu iliyopa ajali ya ndege. Golikipa wa Chapecoense Danilo aliyeokolewa kutoka kwenye ajali ya ndege iliyoanguka Medellin, Colombia alifariki baada ya kuvuja na kupoteza damu nyingi sana ndani na pia kuharibika viungo vyake. Alifikishwa hospitali akiwa amevunjika miguu yote, mikono, mbavu tatu huku figo yake ikiwa imeharibika. Inasemekana kabla ya kufariki alisema maneno haya: “Yesu itazame familia yangu kisha chukua uhai wangu haraka. Tayari baadhi ya rafiki zangu wananisubiri mbinguni, wanahitaji golikipa huko walipo.”
Martial ataitia hasara Man United endapo ataendelea kufunga Ulikuwa ni usiku mzuri kwa upande wa mshambuliaji wa Manchester United Anthony Martial. Mfaransa huyo alionekana kurejea kwenye ubora wake kenye kikosi cha Jose Mourinho na kufanikiwa kutupia bao mbili kambani. Bao la kwanza alitengenezewa na Henrikh Mkhitaryan, Martial alifunga bao la pili kwa kuunganisha krosi kutoka kwa Antonio Valencia. Mabao hayo mawili yaliisaidia Manchester United kupata ushindi wa magoli 4-1 ushindi uliosherekewa baada ya dakika 90. Wakati Martial anasaini mkataba wa kujiunga na Manchester United kulikuwa na baadhi ya vipengele kwenye mkataba huo ambavyo vitaifanya Monaco kuvuna kitita cha pesa endapo Martial atakuwa akifanya vizuri akiwa Manchester United. Hadi sasa Martial ameshafunga magoli 20 pamoja na magoli mawili aliyofunga kwenye mchezo dhidi ya West Ham. Kama atafunga magoli mengine matano, Manchester United watatakiwa kuilipa Monaco €10,000,000 wakiongeza kwenye kiasi ambacho tayari walilipa wakati wanamsainisha mkataba mwaka uliopita.
Arsenal yasukumwa nje ya EFL Magoli ya Jordy Clasie na Ryan Bertrand yameitupa nje Arsenal kwenye kombe la EFL na kuipeleka Southampton hatua ya nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1987. Kocha wa Arsenal Arsene Wenger ambaye hajawahi kutwaa taji hilo katika miaka yake 20 aliyoishi London, alifanya mabadiliko ya wachezaji 10 kwenye kikosi cha Arsenal kilichoshinda 3-1 dhidi ya Bournemouth kwenye mchezo wa Premier League Jumapili iliyopita. Southampton ambao wameshinda mara moja katika michezo 23 waliyosafiri kuifata Arsena, walistahili ushindi na watacheza dhidi ya Liverpool kwenye mchezo wa nusu fainali ya kwanza itakayochezwa kwenye uwanja wa St Mary January 9 mwaka ujao.
Man United 'kulipiza kisasi' dhidi ya West Ham Kiungo wa kati Paul Pogba na Marouane Fellaini watakosa mechi ya kulipiza kisasi ya robo fainali dhidi ya West Ham baada ya kuhudumia marufuku. Wote wawili walipewa kadi za njano kwa mara ya tano msimu huu wakati timu yao ilipopata sare ya 1-1 siku ya Jumapili. Mshambuliaji wa West Ham Diafra Sakho ,ambaye alifunga bao katika uwanja wa Old Trafford wikendi iliopita anauguza jeraha la kifundo cha mguu. Anday Caroll yuko karibu kurudi katika kikosi cha kwanza baada ya kuuguza jeraha la goti huku beki Winston Reid akirudi baada ya kuhudumia marufuku. Kiungo wa kati wa Manchester United Ander Herrera amesema kuwa itakuwa mechi ya ''kulipiza kisasi'' baada ya timu yake kufeli kuishinda West Ham wikendi iliopita. Katika mechi nyengine Arsenal itaikaribisha West Ham katika uga wa Emirates
Gareth Southgate ndio kocha rasmi wa Uingereza Gareth Southgate amechaguliwa rasmi kuwa kocha wa Uingereza katika mkataba wa kudumu. Southgate mwenye umri wa miaka 46 aliwacha wadhfa wake kama mkufunzi wa timu ya Uingereza ya vijana wasiozidi miaka 21 mnamo mwezi Septemba baada ya aliyekuwa meneja wa Uingereza Sam Allardyce kujiuzulu baada ya kuhudumu kwa siku 67 pekee. Aliisaidia Uingereza kushinda mara mbili pamoja na sare mbili kama kaimu mkufunzi na sasa ametia saini kandarasi ya miaka minne yenye thamani ya pauni milioni 2 kwa mwaka. ''Nimefurahia sana kushirikiana na wachezaji katika mechi nne na ndhani kuna vipaji vingi'',alisema.
MILEN MAGESE AAHIDI USHIRIKIANO NA SERIKALI ILI KUSAIDIA VIPAJI VYA UREMBO Mkurugenzi wa Kampuni ya Millen Magese Group (MMG), Millen Magese ameishukuru Serikali kupitia kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye, huku akifurahishwa na uwakilishi mzuri wa Miss Tanzania Julitha Kabete (19), aliyeingia kwenye tano bora katika mashindano ya Afrika. Kabete alipeperusha vema Bendera ya Tanzania kwa kuingia hatua ya tano bora ya mashindano yaliyofanyika Jumamosi nchini Nigeria na kuitoa Tanzania kimasomaso. Akizungumza na waandishi wa habari, Millen alisema ni faraja kubwa kwake na nchi yake kwa Julitha kuingia hatua ya tano bora, lakini sababu kubwa ikiwa ni ushirikiano iliyoupata. "Napenda kuchukua fursa hii kwa heshima nyingi na taadhima kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa ushirikiano wa hali ya juu, kupitia Waziri Nape Nnauye kwa ushirikiano na mwongozo wa kipekee, wazazi na familia nzima ya Julitha kwa malezi yenu kwa binti , Kamati nzima ya Miss Tanzania chini ya Mkurugenzi Hashim Lundenga (Tunashukuru sana), kwenu wanahabari hatuna maneno sahihi ya shukrani, asanteni sana," alisema Magese. Naye mshindi huyo wa tano wa Miss Afrika, Julitha Kabete, alisema anashukuru kwa ushirikiano aliupata, lakini pia nchi yake kupata thamani ya kipekee katika shindano hilo kupata nafasi tano za juu. Kabete alisema kuwa licha kutopata nafasi ya kwanza, lakini ameweza kuiwakilisha vema nchi katika shindano hilo, kwa sababu ushindani ulikuwa mkali sana. "Kwangu ni faraja kubwa kwa kuwa balozi mzuri wa Tanzania na kuweza kuwashinda wenzangu wengi ikiwemo na mwenyeji wetu ambaye hakuingia katika hatua ya tano kama ambayo mimi nimeipata nina furaha kubwa sana,"alisema Kabete. Alisema kuna mkataba mpya ambao utaingiwa kati ya Tanzania na waandaaji wa shindano hilo la Miss Africa katika kutoa ushirikiano wa ushiriki wa shindano hilo. Katika shindano hilo lililofanyika Novemba 26, mwaka huu nchini Nigeria, taji la shindano hilo lilienda kwa mnyange Neurite Mendes (23) wa Angola, aliyenyakua kitita cha dola za Marekani 25,000 sawa na sh.milioni 52 ya Kitanzania na gari jipya (brand new 2016 Ford Escape), safari maalum ya mafunzo nchini Uingereza na Ubalozi wa Mazingira– Afrika. Mshindi wa pili katika shindano hilo ni Refilwe Mthimunye wa Afrika Kusini alipata dola za Kimarekani 15, 000 ni sawa na zaidi ya sh. milioni 32, na Jencey Anwifoje kutoka nchini Cameroon, akiibuka wa tatu na kupata dola za kimarekani 10,000 sawa na zaidi ya sh.milioni 20. Shindano la Miss Afrika 2016 lilichagizwa kwa heshima ya mji wa Calabar na jimbo la Cross River, chini ya Gavana wa Cross River Profesa Ben Ayade. Kampuni tanzu ya Millen Magese (MMG) imeanzishwa kwalengo la kuibua, kuinua, kutambua na kukuza vipaji katika Bara la Afrika na ngazi ya Kimataifa. MMG imeweza kufika nchi mbalimbali barani Afrika na mwaka 2012 iliweza kuendesha shindano la kwanza ya aina yake ambapo wanamitindo wawili kutoka Tanzania walipata nafasi ya kupata mikataba nchini Afrika Kusini. Wanamitindo kutoka mashindano hayo wameweza kuendelea kufanya vizuri maonesho mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. Mwaka huo huo wa 2012 MMG kupitia mradi wa TIFEX iliwezesha wabunifu kutoka nchini kupata uzoefu na uelewa wa wiki za mitindo duniani.
TFF YATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI BRAZIL, NI ILE AJALI ILIYOTEKETEZA TIMU YA SOKA Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametuma salamu za rambirambi kwa Shirikisho la Mpira Brazil (CBF), kutokana na vifo vya wachezaji wa timu ya soka Chapecoense Real ya Brazil. Rais wa TFF Malinzi, katika salamu za rambirambi kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Brazil (CBF), Lucca Victorelli amesema ajali hiyo iliyoua watu wengi ni tukio la kusikitisha kwenye familia ya soka duniani na limetokea katika kipindi kigumu. Rais Malinzi ambaye alituma salamu hizo pia kwa mashabiki wa Chapecoense na Jumuiya ya soka na wanafamilia wengine wa nchini Brazil, amesema: “Mawazo yetu yapo kwa wahanga wa ajali hiyo, familia na jamaa zao.” Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri juzi Jumatatu kutoka Brazil kupitia Bolivia kwenda Colombia ilibeba abiria 81 wakiwamo wafanyakazi na wachezaji wa Chapecoense Real ya Brazil kabla ya kuanguka kwenye milima ya Colombia. Wachezaji hao wa Chapecoense Real ya Brazil walikuwa wakisafiri kwenda kucheza mechi ya fainali ya michuano ya ubingwa wa Kombe la Amerika ya Kusini (Copa Sud Americana). Walikuwa ni miongoni mwa abiria 81. Michuano hiyo ni ya pili kwa ukubwa katika Bara la Amerika ya Kusini, iliyotarajiwa kuchezwa leo Jumatano Novemba 30, 2016 ambako Chapecoense Real ingecheza dhidi ya Atletico Nacional ya Colombia. Ndege hiyo ilikuwa imebeba wachezaji wa timu ya Chapecoense Real ya Brazil, awali ilitoa taarifa ya hali ya hatari iliyosababishwa na hitilafu kwenye mfumo wa umeme, na hatimaye kuanguka muda mfupi baadaye karibu na mji wa Medelin. Taarifa za vifo hivyo, zimethibitishwa na Mkuu wa Mamlaka ya Anga ya Brazil, Alfredo Bocanegra aliyesema walionusurika ni Watu watano wakiwamo wachezaji watatu wa Chapecoense na wafanyakazi wawili wa ndege hiyo.
KIPYA MPYA MGHANA ATUA DAR ES SALAAM KUJIUNGA NA SIMBA Baada ya awali kuonyesha nia ya kuhitaji kipa mpya, hatimaye kipa Daniel Agyei amewasili rasmi nchini tayari kujiunga na kikosi cha Simba. Mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar, kipa huyo alipokelewa na Mratibu wa Simba, Abbas Ally. Simba itafanya mazungumzo na kipa huyo raia wa Ghana ambaye pia ni kipa namba moja wa kikosi cha Medeama cha Ghana lengo ni kuongeza ushindani kwenye nafasi hiyo. "Ndiye anaonekana kuwa chaguo sahihi, kazi yake ilionekana akiwa kwenye Kombe la Shirikisho," kilieleza chanzo. Kocha Joseph Omog alipendekeza kuongezwa kwa kipa mmoja ili ‘kumbusti’ Vicent Angban.
Wacha nifunguke Uamuzi wa kutumia busara badala ya sheria na kanuni TFF mnautoa wapi? Huu utaratibu wa kutumia busara katika kufanya maamuzi ya kisheria na kanuni tumeutoa wapi? Taratibu zinajulikana, sheria zipo, kamati husika ipo, kilichokuwa kinatakiwa ni kulishughulikia jambo hili kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni kwa kuzingatia ushahidi wa pande zote mbili ili upande wenye haki upewe haki yake. Kuna faida mbili kama kamati ingesimama katika sheria kuliko kuipeleka kesi hii kishkaji na siasa za Simba na Yanga. Faida ya kwanza kama kesi hii ingeamuliwa kisheria ni kuijengea heshima na imani TFF na mamlaka husika kwa kusimama kwenye haki pasipo kuyumba na kutoa fundisho au angalizo kwa wengine kwamba taasisi haiyumbishwi imesimama kwenye mstari. Jambo la pili ni kutengeneza mazingira ya kuwasaidia wachezaji wenyewe kwamba hata kama wanafanya ujinga wa kufanya udanganyifu na kusaini timu mbili au kusaini timu nyingine wakati bado mikataba yao na timu nyingine ipo hai watakua wakijua lazima watakabiliwa na adhabu bila kujali ni wachezaji wa Simba au Yanga. Lakini inapofika wakati TFF inatoa nafasi kwa vilabu kumalizana nje ya sheria wanakuwa hawatatui tatizo la muda mrefu, vipi mambo hayo yakifanywa na vilabu kama Ruvu Shooting na Mbao FC? Msimu ujao huenda Simba wakamsajili mchezaji wa Yanga kimagumashi TFF haitakuwa na meno ya kuiadhibu Simba moja kwa moja kwasababu Yanga walipofanya hivyo TFF ilitoa nafasi kwa vilabu kumalizana kisela. Jana afisa habari wa TFF Alfred Lucas aliutangazia umma wa watanzania kwamba, kesi hiyo imerudishwa kwenye kamati ya sheria na hadhi za wachezaji kwa ajili ya kufanyiwa uamuzi, TFF imeiagiza Simba kupeleka mkataba halali waliosainiana kati ya Simba na Hassan Ramadhani Kessy pamoja na ushahidi unaothibisha kwamba Simba walikuwa wanamlipa Kessy hususan katika miezi mitatu ya mwisho. Sasahivi kesi imegeuka, mwanzo Simba walilalamika kuwa Kessy alivunja mkataba kwa kuanza kuitumikia Yanga wakati bado alikuwa na mkataba halali na klabu ya Simba. TFF badala ya kuamua Kessy ya msingi sasahivi inataka kujiridhisha kama Kessy alikuwa akilipwa mshahara au la! Mbona Kessy hakufungua kesi ya kuidai Simba? Kwahiyo, kama mchezaji akiwa anaidai klabu mishahara inabidi asajiliwe na klabu nyingine bila kufuata taratibu? Kwa mujibu wa taarifa za Simba, Kessy alibakiza siku chache ili mkataba wake na Simba umalizike, lakini hiyo haimaanishi mchezaji alitakiwa avae jezi za Yanga, kusafiri au kuhusika moja kwa moja na shughuli za Yanga ilibidi asubiri hadi mkataba wake umalizike. Baada ya Yanga kuona wamefanya kosa huenda Kessy aliwaambia makataba wake na Simba umemalizika lakini wao hawakujiridhisha, wanatafuta sehemu ya kusawazisha ndiyo maana wanaomba ushahidi (salary slip au bank statement) wa malipo ya mishahara ya Simba kumlipa Kessy. Sasa kama Simba walikuwa wanamlipa Kessy kishkaji kwa kutoa pesa mfukoni bila maandishi watashindwa kwenye kesi hii kwasababu wakishindwa kuthibitsha kwamba walikuwa wanamlipa Kessy kwa zaidi ya miezi mitatu, basi moja kwa moja mkataba utakuwa ulivunjwa na Simba wenyewe. Ngoja tuendelee kujionea sarakasi za Simba na Yanga kwenye soka la Tanzania huku jaji wao akiwa ni kipofu.
Klabu yatoa first xi ya kikosi chao kuwapa Chapecoense Club Libertad wamejitolea wachezaji wao wote wa kikosi cha kwanza kuwapa timu ya Chapecoense kufuatia ajali mbaya ya ndege waliyopata timu hiyo ambapo watu 76 kati ya 81 wamefariki dunia. Wakiwa njiani kusafiri kuelekea kwenye mchezo mkali na wa kihistoria kwao, klabu ya Chapecoense ilikuwa icheze mchezo wa fainali ya Copa Sudamericana dhidi ya Atletico Nacional lakini kufika njiani maafa yaliwakuta. Klabu hiyo ya Paraguay ‘Club Libertad’ walifungwa na kutupwa nje ya mashindano na Chapecoense kwa mikwaju ya penati katika hatua ya roo fainali ya michuano hiyo. Taarifa kutoka klabu hiyo inasomeka hivi; “Uongozi na timu nzima ya Club Libertad unaungana na wahanga kutoa salamu za rambirambi, kutokana na maafa yaliyowakuta ndugu zetu wa klabu ya ASOCIACION CHAPECOENSE DE FUTBOL na kuamua kutoa wachezaji wote wa kikosi cha kwanza kwa Chapecoense endapo kutakuwa na tukio lolote la kimichezo kwenye nchi yao. Tutoa pole kwa pigo la kuondokewa na wachezaji muhimu si tu kwa klabu bali kwa taifa pia
DONEDEAL: Ngasa kasaini Mbeya City Picha inayo-trend kwa sasa kwenye mitandao ya kijamii ni ya Mrisho Ngasa na afisa habari wa Mbeya City Dismas Ten ambayo inaashiria tayari nyota huyo wa zamani wa Yanga ameshakamilisha deal na ‘wagonga nyundo wa Mbeya’ Mbeya City. Mwezi Septemba mwaka huu Ngasa alijiunga na Fanja FC inayoshiriki ligi kuu nchini Oman (Oman Professional League) ikiwa ni wiki tatu tu, baada ya kuvunja mkataba na klabu ya Free State Stars ya South Africa. Nyota huyo wa zamani wa vilabu vya Kagera Sugar, Yanga, Azam FC na Simba vyote vya VPL hajadumu Oman na hatimaye amerejea tena nchini na kusajiliwa na klabu ya Mbeya City ambapo ataungana na kocha wake wa zamani Kinna Phiri aliyemsajili kutoka Yanga kwenda Free State Stars kabla ya kocha huyo kutimuliwa kufatia mfululizo wa matokeo mabovu. Afisa habari wa Mbeya City Dismas Ten ame-post picha kwenye ukurasa wake wa Instagram akiwa pamoja na Mrisho Ngasa na kuandika maneno yanosomeka: “Mnapokamilisha jambo kutakiana heri ndio uungwana. Kila la heri anko @mrisho_ngasa_17.” Habari za Ngasa kujiunga na Mbeya City zilianza tangu aliporejea nchini akitokea South Africa baada ya kuvunja mkataba na Free State lakini ghafla akaibukia Oman na kusajiliwa na Fanja FC siku chache baada ya klabu hiyo kumsajili mtanzania mwingine Danny Lyanga mshambuliaji wa zamani wa Simba. Jana jioni zikaenea tena habari kwamba Mbeya City wameshakamilisha usajili wa Ngasa. Lakini uongozi wa klabu hiyo haukuwa tayari kuthibitisha badala yake ukasema utatoa taarifa rasmi, mwisho wa siku raundi ijayo ya VPL Ngasa atakuwa miongoni mwa wachezaji watakaokipiga Mbeya City.
KAGERA WAMEMSIMAMISHA CASILLAS, HALAFU WAMEMPOTEZEA Kipa Kagera Sugar aliyesimamishwa na uongozi wa timu hiyo kupisha uchunguzi wa madai ya kuuza mechi, Hussein Shariff ‘Casillas’, amefunguka kuwa mpaka sasa yupo nyumbani na hakuna kiongozi yeyote yule ambaye amemfuata kwa ajili ya kulizungumzia suala hilo. Casillas ambaye amewahi kuidakia Simba kwa msimu mmoja, alisimamishwa na uongozi wa timu hiyo inayonolewa na Mecky Maxime akiwa sambamba na beki Erick Kyaruzi baada ya timu hiyo kufungwa mabao 6-2 na Yanga kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza. Kipa huyo ambaye amebakiza mkataba wa miezi sita na timu hiyo, amesema tangu aliposimamishwa amekuwa nyumbani bila ya kufahamishwa chochote na viongozi hao juu ya hatima yake ya kurejea katika kikosi hicho. “Mpaka sasa nipo nyumbani na sijui chochote kinachoendelea juu yangu kuhusiana na kurejea katika timu kwa sababu sijaambiwa wala sijataarifiwa lolote na viongozi tangu ambapo waliponisimamisha katika mzunguko wa kwanza. “Na mkataba wangu sasa umebakia miezi sita pekee ya kuendelea kukipiga katika kikosi hicho lakini hata hivyo sitaki kuliongelea kwa undani suala hilo, nawasubiria wao juu ya uamuzi ambao watakuja kuutoa,”alisema Casillas ambaye aliwahi kuwa kipa bora msimu wa 2014/15.
Jumanne, 29 Novemba 2016
WAZIRI MWIGULU AKUTANA NA ZULU, NI YULE KIUNGO MPYA ALIYETUA DAR USIKU WA MANANE Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba ambaye ni shabiki wa Yanga wa ‘kugalagala’, amekutana na kiungo mpya wa Yanga, Justice Zulu. Zulu raia wa Zambia, yuko nchini tayari kumalizana na Yanga. Mwigulu ambaye ni straika tegemeo wa Yanga katika timu ya Wabunge ameonekana akiwa picha na Zulu, nje ya hoteli aliyofikia. Zulu anatarajia kumalizana na Yanga, leo au kesho na mara moja ataanza kazi katika harakati za kocha mpya, George Lwandamina kuandaa kikosi chake
HIVI NDIVYO KASSIM DEWJI ALIVYOZUIA AWADHI JUMA KUPELEKWA KWA MKOPO Uliisikia hii taarifa? Imeelezwa kuwa kigogo mmoja wa klabu ya Simba, jina kapuni amezuia uhamisho wa mchezaji Awadhi Juma ambaye alitakiwa kupelekwa kwa mkopo katika timu ya Kagera Sugar katika usajili huu wa dirisha dogo kwa madai ya kiwango chake kushuka. Awadhi ni miongoni mwa wachezaji kadhaa wa Simba ambao hawakupata nafasi ya kucheza mechi hata moja katika mzunguko wa kwanza wa ligi kuu kutokana na kocha Joseph Omog kutompanga katika kikosi chake. Chanzo kutoka Simba ambacho hakikutaka kuweka wazi jina lake kimeeleza kuwa, kuna baadhi ya viongozi walikuwa katika mipango ya kumtoa kwa mkopo kiraka huyo kwenda Kagera Sugar lakini jaribio lililogonga mwamba. “Awadhi ni miongoni mwa wachezaji ambao walikuwa kwenye mipango ya kutolewa kwa mkopo katika usajili wa dirisha dogo kutokana na kutopata nafasi ya kucheza mzunguko wa kwanza. “Maamuzi hayo yalipingwa vikali na kigogo mmoja wa Simba kufuatia kuutambua vilivyo uwezo wake kutokana na kuwa mchezaji muhimu katika timu hiyo, lakini pia ni kwa kuwa anaweza kucheza namba nyingi uwanjani,” kilisema chanzo hicho.
BAADA YA MZUNGUKO WA KWANZA, MAHADHI AWEKA WAZI KUCHOSHWA NA BENCHI LA YANGA Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Juma Mahadhi, amefunguka kwamba amechoshwa na maisha ya kukaa benchi katika kikosi hicho na katika mzunguko huu wa pili anajifua vilivyo kuhakikisha anaingia katika kikosi cha kwanza. Mahadhi aliyejiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu huu akitokea Coastal Union ya Tanga, amekumbana na ushindani mkubwa mbele ya viungo wenzake Simon Msuva na Geofrey Mwashiuya jambo ambalo linasababisha atumike kama chaguo la mwisho mbele ya nyota hao. Akionyesha kujiamini, Mahadhi amesema ameamua kuja kitofauti kwa ajili ya kujihakikishia namba ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha Mzambia, George Lwandamina ambapo atajitahidi kuongeza juhudi ili kupata nafasi hiyo. “Sasa hali ya kutocheza mara kwa mara imenichosha kwani nahitaji nafasi ya kuonyesha mchango wangu kwenye timu ambapo nimepanga katika mzunguko huu wa pili nijifue zaidi kwa ajili ya kuliaminisha benchi la ufundi na wanipe nafasi hiyo. “Najua kwamba haitakuwa kazi rahisi kwani ninaoshindana nao ni watu wenye viwango vikubwa kama mimi lakini hilo halitanifanya nikate tamaa kwani lengo langu ni kuona nacheza mara kwa mara,” alisema Mahadhi.
USAJILI KIUNGO MPYA AZAM FC WAMSUBIRI KOCHA MHISPANIA AREJEE Kutokana na kutokuwepo nchini kwa Kocha Mkuu wa Azam, Zeben Hernandez, dili la klabu hiyo kumsajili kiungo wa Mbeya City, Joseph Mahundi limekwama mpaka atakaporejea kocha huyo kutoka Hispania. Mahundi ambaye alikuwa akifukuziwa kwa muda mrefu na Azam kwenda kusaidia safu ya kiungo mshambuliaji, atajiunga na Azam akiwa huru baada ya mkataba wake na Mbeya City kumalizika. Meneja wa mchezaji huyo, Herry Chibakasa ‘Mzozo’, amesema tayari wameshafanya mazungumzo ya awali, lakini kinachochelewesha dili hilo ni kutokuwepo kwa kocha huyo mkuu ambapo Azam imesema haitaki kufanya usajili bila ya uwepo wake. “Kila kitu kinaenda sawa, tayari tushafanya mazungumzo ya awali na yameenda vizuri, mchezaji wangu huyu yupo huru kutokana na mkataba wake kumalizika, hivyo naamini hakuna kipingamizi cha yeye kushindwa kujiunga na Azam kama taratibu zikifuatwa. “Mpaka sasa ishu haijakamilika kutokana na kwamba makocha wao hawapo hasa mkuu kwani Azam wanataka usajili unapofanyika na wao wawepo, hivyo wamesema anarudi Desemba 2, ndiyo tutamaliza dili hilo,” alisema Mzozo. Mpaka sasa Azam imeshakamilisha usajili wa wachezaji watatu wa kigeni ambao ni Enock Atta Agyei, Samuel Afful na Yahaya Mohammed wote kutoka Ghana.
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)