AZAM FC YAZINDUKA, YAILAZA 1-0 PRISONS CHAMAZI Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, usiku wa jana imeiadabisha Tanzania Prisons kwa bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam. Mchezo huo ulikuwa ni wa mwisho kwa Azam FC mwaka huu kabla ya kuukaribisha mwaka mpya ‘2017’, bao hilo pekee limewekwa kimiani na nahodha John Bocco ‘Adebayor’, dakika ya 40 baada ya kupokea pasi safi ya Joseph Mahundi na kuwahadaa mabeki wa Prisons kisha kupiga shuti la kiufundi lililojaa kimiani. Azam FC iliingia kwenye mchezo huo ikiwa na sura mpya kwenye benchi la ufundi lililosimamiwa na makocha wa timu yake ya vijana, Idd Nassor 'Cheche' na Idd Abubakar na hii ni kufuatia kuwasitishia mikabata wakufunzi kutoka Hispania wakiongozwa na Kocha Mkuu, Zeben Hernandez. Hiyo inamaanisha kuwa makocha hao wa muda wameanza kibarua chao vema kwa kujiandikia rekodi ya kuiongoza Azam FC kushinda mchezo wa ligi katika mechi yao ya kwanza wakiwa benchini. Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii waliuanza mchezo huo vema wakifanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Prisons, lakini safu yao ya ulinzi ilikuwa imara kuondoa hatari zote wakiongozwa na Salum Kimenya. Alikuwa ni Bocco aliyeihakikishia Azam FC bao la uongozi hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika. Kipindi cha pili Azam FC iliongeza nguvu kwa kuwaingiza Shaaban Idd, Himid Mao na Samuel Afful, lakini jitihada za kusaka mabao zaidi zilishindikana kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya Prisons. Kiungo Frank Domayo, alikaribia kuipatia bao la pili Azam FC dakika ya 50 akiwa anatazamana na kipa wa Prisons, lakini shuti aliloopiga lilitoka pembeni kidogo ya lango la wapinzani wao. Dakika moja baadaye mshambuliaji wa Azam FC, Yahaya Mohammed, alifanya jitihada binafsi za kuwatoka mabeki wa Prisons lakini shuti alilopiga lilitoka nje ya lango la Prisons. Prisons ilipata pigo dakika ya 69 baada ya kiungo wao mkabaji, Kazungu Mashauri, kuonyeshwa kadi nyekundu kufuatia kumfanyia madhambi ya makusudi winga wa Azam FC, Mahundi ambaye alishindwa kuendelea na mchezo huo na nafasi yake kuchukuliwa na nahodha msaidizi, Himid Mao. Hadi dakika 90 zimalizika ubao wa matokeo ulikuwa ukisomeka vilevile na hivyo kufanya Azam FC kuondoka na pointi zote tatu zinazoifanya kufikisha jumla ya pointi 30 katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikizidiwa pointi 14 na kinara Simba (44) na 10 kwa upande wa Yanga waliojikusanyia 40. Huo ni ushindi wa kwanza wa Azam FC kwenye mechi za mzunguko wa pili wa ligi baada ya kuanza vibaya kwa kutoka sare mechi mbili mfululizo dhidi ya African Lyon (0-0) na Majimaji (1-1). Azam FC kwa sasa inaelekea kwenye changamoto nyingine ya kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambapo itaanza kufungua dimba Jumatatu ijayo kwa kucheza na Zimamoto saa 10.15 jioni ndani ya Uwanja wa Amaan, visiwani Zanzibar. Kikosi cha Azam FC leo; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Stephan Kingue, Salum Abubakar, Frank Domayo, Yahaya Mohammed/Shaaban dk 64, John Bocco/Samuel Afful dk90, Joseph Mahundi/Himid dk 71.

Alhamisi, 29 Desemba 2016

NGASSA SASA RUKSA KUCHEZA MBEYA CITY, ITC YAKE YAFIKA Na Mwandishi Wetu, MBEYA KIUNGO Mrisho Khalfan Ngassa sasa yuko huru kuchezea klabu yake mpya, Mbeya City ya hapa baada ya kupatiwa Hati yake ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC). Mwenyekiti wa Mbeya City, Mussa Mapunda ameiambia Bin Zubeiry Sports - Online leo kwamba ITC ya Ngassa aliyekuwa anachezea Fanja ya Oman imefika nchini asubuhi ya leo. Mapunda amesema kwamba anawashukuru Fanja, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Chama cha Soka Oman (OFA) ambao kwa pamoja wamefanikisha kupatikana kwa ITC hiyo. Mrisho Ngassa sasa yuko huru kuchezea Mbeya City baada ya kupatiwa ITC yake “Ni kweli tumeipata, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Shirikisho la Soka nchini, TFF, Chama cha Mpira cha Oman, hakika wamefanya kazi kubwa kufanikisha kupatikana kwa ITC hii na pia naishukuru Fanja FC na watendaji wote kwenye timu yetu, tumekuwa na mawasiliano mazuri muda wote mpaka tumefanikiwa,” alisema. Mapunda alisema kwamba kuchelewa kufika kwa ITC hiyo hakukuwa na msuguano wowote baina ya klabu hizo mbili, bali kilichokuwa kinatokea ni tofauti ya wakati na siku za ufanyaji kazi kwenye ofisi kulingana na taratibu za nchi hizo mbili, yaani Oman na Tanzania. “Hakukuwa na msuguano wowote uliosababisha kuchelewa kwa ITC hii, kilichokuwepo ni utofauti wa taratibu za kiofisi, mara nyingi Oman siku za Ijumaa na Jumamosi inakuwa ni mapumiko na huku kwetu Jumapili inakuwa mapumziko, hapo ndipo palikuwa panatuletea mpishano, jambo jema ni kuwa tayari tumeipata na tunaweza kumtumia mchezaji kwenye michezo yote ya ligi na mingine ambayo inaihusu klabu yetu,” alisema. Katika hatua nyingine Mapunda alisema kwamba maandalizi kuelekea mchezo wao ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumamosi dhidi ya Mbao FC Uwanja wa Sokoine mjini hapa yanaendelea vizuri na lengo lao ni kushinda baada ya suluhu katika michezo yao miwili iliyopita.

LIVE KUTOKA UWANJA WA UHURU: RUVU SHOOTING VS SIMBA (MAPUMZIKO) MAPUMZIKO GOOOOOOOOO, Mpira wa krosi safi, Mo Ibrahim anaunganisha kwa shuti kali kabisa hapa -Kona safi inachongwa hapa, Banda anajitishwa vizuri hapa. Goal kick -Simba wanaingia vizuri kabisa, Zimbwe anapiga krosi lakini Makwaya anaokoa, konaaa DAKIKA 3 ZA NYONGEZA Dk 45 sasa, mpira mwingi unachezwa katikati zaidi Dk 43, nafasi nyingine kwa Simba, MZamiru anauwahi mpira ukizagaa anaachia shuti kali lakini unapita juuuu KADI Dk 41, kipa Bidii Hussuein analambwa kadi ya njano kwa kupoteza muda Dk 40, Simba wanapoteza nafasi nyingine ya wazi, Pastory anashindwa kulenga KADI Dk 38, Jabir Aziz Stima analambwa kadi ya njano kwa kumrushia daruga Athanas Dk 36, mkwaju wa adhabu wa Abdi Banda unapigwa na kupaa juu ya lango DK 32, Zimbwe anaingia vizuri lakini JKT wanakuwa wepesi kuokoa Dk 29, Shooting wanafanya shambulizi kali hapa, kona. Hii ni kona ya kwanza ya Ruvu leo Dk 26, Mo Ibarahim anaachia mkwaju mkali lakini Juhudi anadaka kwa ustadi mkubwa hapa Dk 20, Ruvu wanaonekana kuwa na kasi zaidi na kuanza ksuhambulia kwa kasi zaidi DK 14, krosi safi, mpira unapigwa na kugonga mwamba. Lakini sasa kipa wa Ruvu yuko chini akitibiwa Dk 13, Mo Ibra anaingia vizuri hapa ndani ya 18, Ruvu wanaokoa na kuwa konaaaaa Dk 11, mpira umesimama hapa Kisiga akiwa anatibiwa hapa Dk 9, Simba wanafanya shambulizi la haraka, Mwanjale anapanda akigongeana na wenzake, anatoa krosi safi kwa Pastory, yeye na nyavu anapaishaa buuuuu Dk 6, Simba wanaendelea kulisakama lango la Ruvu, Mo Ibra anaingia vizuri na kupiga shuti kali, kipa anadaka mpira unamtoka lakini anawahi Dk 4, krosi nzuri ya Kichuya, Athanas anaunganisha tena, lakini Shooting wanaokoa Dk 2, krosi safi ya Zimbwe, Athanas anapiga kichwa hapa lakini ni goal kick Dk 1, Simba wanaanza kwa kasi wakionekana wamepania kupata bao KIKOSI CHA SIMBA 1. Daniel Agyei 2. Besaka Bukungu 3. Mohammed Hussein 4. Abdi Banda 5. Method Mwanjale 6. Jonas Mkude 7. Shiza Kichuya 8. James Kotei 9. Pastory Athanas 10.Muzamiru Yassin 11. Mohammed Ibrahim