Jumamosi, 3 Desemba 2016

MZEE MZIMBA AFARIKI DUNIA KIONGOZI wa zamani wa klabu ya Yanga, Yussuf Mzimba amefariki dunia Alasiri ya leo mjini Dar es Salaam. Mtoto wa marehemu, Ramadhani Yussuf Mzimba ‘Kampira’ ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba baba yao amefariki katika hospitali ya Mwananyamala alipopelekwa kwa matibabu. “Mzee kwa muda alikuwa anasumbuliwa na maradhi ni kwa sababu ya utu uzima. Tulimpeleka hospitali leo kwa matibabu, akatibiwa, akaachwa apumzike na wakati amepumzika ndiyo umauti ukamfika,”amesema. Kampira amesema Mzee Mzimba alikwenda hospitali akitokea nyumbani kwa mwanawe mkubwa, Khalid eneo la Magomeni Kondoa na hapo ndipo msiba wake utakapowekwa. Mazishi yanatarajiwa kufanyika kesho, lakini taratibu zote zitataolewa leo baada ya kikao cha kifamilia. Mzimba amefariki dunia akiwa ana umri wa miaka 84 na enzi za ujana wake alikuwa Katibu Mwenezi wa Yanga miaka ya 1970 chini ya Mwenyekiti, Tarbu Mangara (marehemu pia). Ni sehemu ya viongozi waliofanikisha ziara maarufu za nje za klabu hiyo, Brazil mwaka 1973 na Romania mwaka 1978. Baada ya hapo, akaibuka kama mwanaharakati mwishoni mwa miaka ya 1990 kupinga timu hiyo kugeuzwa Kampuni. Alipambana na uongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti Tarimba Abbas na baadaye chini ya Francis Kifukwe kabla ya kupatanishwa na Mwenyekiti wa sasa, Yussuf Manji. Baada ya suluhu hiyo Mzimba akawa miongoni mwa Wazee wa heshima wa Yanga kabla ya kujiweka kando na shughuli za klabu mwaka 2013 kufuatia kuanza kusumbuliwa kiafya. Mungu ampumzishe kwa amani Mzee Mzimba. Amin.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni