Ijumaa, 2 Desemba 2016

Simlaumu Ngasa kusaini Mbeya City, namlaumu kulazimisha kuondoka Afrika Kusini Na moses j mponda MARA baada ya kushinda taji lake la Tatu la ligi kuu Tanzania Bara msimu wa 2014/15 akiwa na kikosi cha Yanga SC, kiungo-mshambulizi, Mrisho Ngasa alijiunga na timu ya Free State Stars inayocheza ligi kuu ya Afrika Kusini. Ngasa alisajiliwa kwa mkataba wa miaka mitano na alikuwa na nafasi ya kucheza PSL hadi mwaka 2020 huku akitengeza pesa kutokana na maslahi mazuri wanayopata wachezaji katika soka la Afrika. Jambo la ajabu, badala ya klabu kuvunja naye mkataba-yeye Ngasa ndiye aliyepeleka mapendekezo ya kuvunja mkataba wake na Free State mwezi Septemba, 2016. Hili ndilo linaloniumiza mimi na si uamuzi wake wa kujiunga na Fanja FC ya Oman-Pro League baada ya mkakati wake wa kurejea Yanga kuzimwa hadharani na aliyekuwa kocha wa mabingwa hao mara mbili mfululizo wa VPL, Mholland, Hans van der Pluijm. Kwanini Ngassa alishindwa kudumu Afrika Kusini sehemu ambayo alipata bahati ya kusajiliwa bila majaribio, tena baada ya kucheza kwa miaka 9 mfululizo katika ligi ya juu Tanzania. Ngasa amechezea Kagera Sugar na aliisaidia kuipa taji la kombe la Tusker mwaka 2006, ameshinda mataji matatu ya VPL akiwa mchezaji wa Yanga (2007/08, 2008/09 na 2014/15). Hakupata mafanikio makubwa kiuchezaji katika timu ya Azam FC-japokuwa alishinda tuzo binafsi ya ufungaji bora wa ligi kuu Bara msimu wa 2010/11. Kiuchezaji Ngasa hajashinda mataji mengi zaidi ya Oscar Joshua lakini angalau aliweza kuchuma vyema pesa za Yanga, Azam na Simba SC aliyeichezea msimu wa 2012/13. Yanga imempata mashabiki wa kutosha na mara zote wanamuheshimu hata akiwa katika jezi ya timu pinzani. Ngasa ni kipaji kingine cha aina yake, licha ya umbo lake dogo, Ngasa akiwa katika ubora wake alituonesha ni kiasi anavyoweza kucheza eneo lote la mbele, akihaha na kuwasumbua mabeki ili kuisaidia timu yake kupata ushindi. Afrika ilimshuhudia vizuri wakati alipokuwa katika kikosi cha Taifa Stars katika michuano ya kwanza ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ndani ya Afrika-CHAN-2009, Ivory Coast. Uhamisho wa Ngasa kutoka Yanga na kujiunga na Azam FC katikati ya mwaka 2009 inasemekana ulimpatia mchezaji huyo kitita cha zaidi ya milioni 100, alichota pia pesa ya Simba katika usajili wake wa mkopo akitokea Azam FC, pia aliporejea Yanga, June 2013 akaunti yake iliongezeka. Ngasa, kama ilivyo kwa Juma Kaseja, Shaaban Nditti, Mecky Mexime ni baadhi ya mifano bora kwa wachezaji vijana wa miaka ya sasa. Wametumia vizuri nafasi ya ufahamu wao, nyakati zao kukusanya kiasi cha pesa wakicheza hapahapa Tanzania. Jambo la kumlaumu Ngasa ni kwanini aliondoka Free State wakati hivi sasa soko la Watanzania ndani ya Afrika Kusini linaanza kukua? Baada ya kuwa na msimu mgumu zaidi upande wake kama mchezaji wa Yanga, majeraha ya nyama za paja na kiwango cha juu kutoka kwa Saimon Msuva na msaada mkubwa wa Danny Rwanda msimu wa 2014/15, Ngassa alikuwa akishambuliwa sana, huku maisha yake binafsi yakiripotiwa kummaliza. Nakumbuka wakati ule, Januari 2015 niliandika, Ngasa hajaisha na atarudi kwa kasi na kuwaonyesha watu yeye ni mchezaji wa kiwango cha juu kwa wakati wake. Kuanzia Februari akauwasha moto na kupata dili la kwenda Afrika Kusini baada ya Yanga kumpuuza alipodai mshahara wa dola 3000 kwa mwezi ili asaini mkataba mpya. Wengi walimpongeza kwa uamuzi wake wa kujiunga na Free Stars lakini ameshindwa baada ya kushindwa kukabiliana na ushindani wa namba kikosini. Ajabu baada ya kuvunja mkataba na State akajiunga na Fanja FC ya Oman-Pro League. Ilisemekana, Ngassa alisaini mkataba wa miaka miwili na Fanja lakini sasa baada ya miezi mitatu tunaambiwa amesaini kuichezea City. Katika umri wake wa miaka 27 wala siwezi kumlaumu Ngasa kuichagua City, ama mapenzi yake na Yanga, bali namlaumu kwa kulazimisha kuondoka Afrika Kusini wakati tayari alishacheza VPL kwa miaka 9.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni