pata dondoo mbalimbali za michezo ya ndani na nje ya nchi.mompondazy itakujuza kila kitu.
Ijumaa, 30 Desemba 2016
2016 umekuwa ni mwaka bora kwa mwamuzi Muingereza, Mark Clattenburg, huenda ukawa ni mwaka ambao hatausahau katika career yake. Clattenburg ,41, ndani ya mwaka huu, ameweza kuchezesha michezo ya fainali tatu kubwa, Fainali ya Kombe la FA, Klabu Bingwa Ulaya pamoja na ile ya Euro kule nchini Ufaransa. Kuonesha kuwa huu umekuwa mwaka muhimu kwake, Clattenburg aliamua kuchora Tattoo za Fainali za UCL Milano na Euro 2016 France ambazo alizichezesha.
KOTEI WA SIMBA UTAMWELEZA NINI KUHUSIANA NA WALI MAHARAGE MWANANGU Kiungo mpya wa Simba, James Kotei, amesema kuwa moja ya vyakula ambavyo vinamfurahisha alivyokutana navyo Bongo ni pamoja na wali na maharage. Kotei ametua Simba katika usajili wa dirisha dogo akitokea nchini Ghana kwa lengo la kuongeza nguvu katika nafasi hiyo ikiwa ni pamoja na kuleta ushindani. Kotei ameeleza kuwa alikuwa na kazi kubwa ya kuzoea vyakula vya Tanzania lakini hicho kimepita bila kupingwa katika mwili wake. “Napenda sana wali na maharage, hicho ndicho chakula ninachokipenda kwa hapa tangu nimefika,” alisema Kotei. SOURCE: CHAMPIONI
KALI ONGALA AGOMA KWENDA AZAM, MAJIMAJI CHINI YA GSM YAMSHAWISHI KUBAKI SONGEA Kocha Kali Ongala ataendelea kubaki bosi wa benchi la ufundi la Majimaji. Tayari Kali alikuwa amemalizana na Azam FC na alitarajia kujiunga na timu hiyo leo kwa ajili ya safari ya Zanzibar. Azam FC iliamua kumchukua Kali kwa kuwa imemfukuza kocha wake Zeben Hernandez na jopo zima kutoka Hispania. Lakini Majimaji chini ya uongozi wa kampuni GSM, imefanikiwa kumbakiza Kali. Habari za uhakika kutoka Majimaji zimeeleza, uongozi wa klabu hiyo umefanikiwa kumshawishi Kali kubaki. “Kweli Kali anabaki na ataendelea kuwa kocha wa Majimaji,” kilieleza chanzo. “Juzi aliwaaga wachezaji kwa kuwa alikuwa ameishazungumza na Azam FC. Lakini baadaye uongozi umemuita na umefanikiwa kumshawishi abaki.” Kuhusiana na Kali, Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba alisema bado wako kwenye mazungumzo na Majimaji ili kumtwaa.
AZAM FC YAZINDUKA, YAILAZA 1-0 PRISONS CHAMAZI Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, usiku wa jana imeiadabisha Tanzania Prisons kwa bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam. Mchezo huo ulikuwa ni wa mwisho kwa Azam FC mwaka huu kabla ya kuukaribisha mwaka mpya ‘2017’, bao hilo pekee limewekwa kimiani na nahodha John Bocco ‘Adebayor’, dakika ya 40 baada ya kupokea pasi safi ya Joseph Mahundi na kuwahadaa mabeki wa Prisons kisha kupiga shuti la kiufundi lililojaa kimiani. Azam FC iliingia kwenye mchezo huo ikiwa na sura mpya kwenye benchi la ufundi lililosimamiwa na makocha wa timu yake ya vijana, Idd Nassor 'Cheche' na Idd Abubakar na hii ni kufuatia kuwasitishia mikabata wakufunzi kutoka Hispania wakiongozwa na Kocha Mkuu, Zeben Hernandez. Hiyo inamaanisha kuwa makocha hao wa muda wameanza kibarua chao vema kwa kujiandikia rekodi ya kuiongoza Azam FC kushinda mchezo wa ligi katika mechi yao ya kwanza wakiwa benchini. Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii waliuanza mchezo huo vema wakifanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Prisons, lakini safu yao ya ulinzi ilikuwa imara kuondoa hatari zote wakiongozwa na Salum Kimenya. Alikuwa ni Bocco aliyeihakikishia Azam FC bao la uongozi hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika. Kipindi cha pili Azam FC iliongeza nguvu kwa kuwaingiza Shaaban Idd, Himid Mao na Samuel Afful, lakini jitihada za kusaka mabao zaidi zilishindikana kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya Prisons. Kiungo Frank Domayo, alikaribia kuipatia bao la pili Azam FC dakika ya 50 akiwa anatazamana na kipa wa Prisons, lakini shuti aliloopiga lilitoka pembeni kidogo ya lango la wapinzani wao. Dakika moja baadaye mshambuliaji wa Azam FC, Yahaya Mohammed, alifanya jitihada binafsi za kuwatoka mabeki wa Prisons lakini shuti alilopiga lilitoka nje ya lango la Prisons. Prisons ilipata pigo dakika ya 69 baada ya kiungo wao mkabaji, Kazungu Mashauri, kuonyeshwa kadi nyekundu kufuatia kumfanyia madhambi ya makusudi winga wa Azam FC, Mahundi ambaye alishindwa kuendelea na mchezo huo na nafasi yake kuchukuliwa na nahodha msaidizi, Himid Mao. Hadi dakika 90 zimalizika ubao wa matokeo ulikuwa ukisomeka vilevile na hivyo kufanya Azam FC kuondoka na pointi zote tatu zinazoifanya kufikisha jumla ya pointi 30 katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikizidiwa pointi 14 na kinara Simba (44) na 10 kwa upande wa Yanga waliojikusanyia 40. Huo ni ushindi wa kwanza wa Azam FC kwenye mechi za mzunguko wa pili wa ligi baada ya kuanza vibaya kwa kutoka sare mechi mbili mfululizo dhidi ya African Lyon (0-0) na Majimaji (1-1). Azam FC kwa sasa inaelekea kwenye changamoto nyingine ya kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambapo itaanza kufungua dimba Jumatatu ijayo kwa kucheza na Zimamoto saa 10.15 jioni ndani ya Uwanja wa Amaan, visiwani Zanzibar. Kikosi cha Azam FC leo; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Stephan Kingue, Salum Abubakar, Frank Domayo, Yahaya Mohammed/Shaaban dk 64, John Bocco/Samuel Afful dk90, Joseph Mahundi/Himid dk 71.
Alhamisi, 29 Desemba 2016
NGASSA SASA RUKSA KUCHEZA MBEYA CITY, ITC YAKE YAFIKA Na Mwandishi Wetu, MBEYA KIUNGO Mrisho Khalfan Ngassa sasa yuko huru kuchezea klabu yake mpya, Mbeya City ya hapa baada ya kupatiwa Hati yake ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC). Mwenyekiti wa Mbeya City, Mussa Mapunda ameiambia Bin Zubeiry Sports - Online leo kwamba ITC ya Ngassa aliyekuwa anachezea Fanja ya Oman imefika nchini asubuhi ya leo. Mapunda amesema kwamba anawashukuru Fanja, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Chama cha Soka Oman (OFA) ambao kwa pamoja wamefanikisha kupatikana kwa ITC hiyo. Mrisho Ngassa sasa yuko huru kuchezea Mbeya City baada ya kupatiwa ITC yake “Ni kweli tumeipata, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Shirikisho la Soka nchini, TFF, Chama cha Mpira cha Oman, hakika wamefanya kazi kubwa kufanikisha kupatikana kwa ITC hii na pia naishukuru Fanja FC na watendaji wote kwenye timu yetu, tumekuwa na mawasiliano mazuri muda wote mpaka tumefanikiwa,” alisema. Mapunda alisema kwamba kuchelewa kufika kwa ITC hiyo hakukuwa na msuguano wowote baina ya klabu hizo mbili, bali kilichokuwa kinatokea ni tofauti ya wakati na siku za ufanyaji kazi kwenye ofisi kulingana na taratibu za nchi hizo mbili, yaani Oman na Tanzania. “Hakukuwa na msuguano wowote uliosababisha kuchelewa kwa ITC hii, kilichokuwepo ni utofauti wa taratibu za kiofisi, mara nyingi Oman siku za Ijumaa na Jumamosi inakuwa ni mapumiko na huku kwetu Jumapili inakuwa mapumziko, hapo ndipo palikuwa panatuletea mpishano, jambo jema ni kuwa tayari tumeipata na tunaweza kumtumia mchezaji kwenye michezo yote ya ligi na mingine ambayo inaihusu klabu yetu,” alisema. Katika hatua nyingine Mapunda alisema kwamba maandalizi kuelekea mchezo wao ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumamosi dhidi ya Mbao FC Uwanja wa Sokoine mjini hapa yanaendelea vizuri na lengo lao ni kushinda baada ya suluhu katika michezo yao miwili iliyopita.
SIMBA WALEEE, YANGA WANAISOMA NAMBA...RUVU AFA 1-0 BAO pekee la kiungo Mohammed ‘Mo’ Ibrahim limetosha kuipa Simba ushindi wa 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Ni ushindi huo ambao unaifanya Simba SC ifikishe pointi 44 baada ya kucheza mechi ya 18 na kuendelea kuogoza Ligi Kuu kwa pointi nne zaidi ya mabingwa watetezi, Yanga SC. Mo aliyesajiliwa Simba SC msimu huu kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro, alifunga bao hilodakika ya 45 akimalizia krosi ya beki wa kulia, Janvier Besala Bokungu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Simba ilipata bao hilo, baada ya kukosa mengine zaidi ya matatu ya wazi na pongezi zimuendee kipa chipukizi wa Ruvu Shooting, Bidii Hussein aliyeokoa hatari nyingi.
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)