Msuva anaendelea kuwatesa magolikipa wa Mapinduzi Cup 2017 Simon Msuva ameendelea kuwa bora uwanjani na kuisaidia timu yake kupata ushindi kwenye michuano ya Mapinduzi Cup baada ya kutupia bao mbili kambani na kuifanya Yanga kufikisha pointi 6 na kukaa juu ya Kundi B.
Kama angepata mkwaju wa penati angekuwa mchezaji wa kwanza kufunga hat-trick kwenye mashindano ya msimu huu na kuendelea kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kuibuka mfungaji bora wa michuano ya Mapinduzi 2017.
Msuva alianza kufunga bao la kwanza dakika ya 11 kwa kuiwahi pasi ndefu iliyopigwa na kiungo Thaban Kamusoko, bao lake la pili amelifunga dakika ya 21 bao ambalo limemfanya afikishe magoli manne katika mashindano ya mwaka huu kufuatia kufunga magoli mawili kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Jamhuri wakati Yanga ilipoifunga Jamhuri magoli 6-0.
Hadi sasa Msuva ndiye anaongoza katika orodha ya wafungaji akiwa na magoli manne akifatiwa kwa karibu na Labama mwenye magoli matatu.
January 7 Yanga itacheza na Azam FC mchezo wa tatu katika hatua ya makundi mechi inayosubiriwa kwa hamu na wapenzi wote wa soka kutokana na upinzani uliopo kati ya vilabu hivi viwili.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni