MILEN MAGESE AAHIDI USHIRIKIANO NA SERIKALI ILI KUSAIDIA VIPAJI VYA UREMBO Mkurugenzi wa Kampuni ya Millen Magese Group (MMG), Millen Magese ameishukuru Serikali kupitia kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye, huku akifurahishwa na uwakilishi mzuri wa Miss Tanzania Julitha Kabete (19), aliyeingia kwenye tano bora katika mashindano ya Afrika. Kabete alipeperusha vema Bendera ya Tanzania kwa kuingia hatua ya tano bora ya mashindano yaliyofanyika Jumamosi nchini Nigeria na kuitoa Tanzania kimasomaso. Akizungumza na waandishi wa habari, Millen alisema ni faraja kubwa kwake na nchi yake kwa Julitha kuingia hatua ya tano bora, lakini sababu kubwa ikiwa ni ushirikiano iliyoupata. "Napenda kuchukua fursa hii kwa heshima nyingi na taadhima kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa ushirikiano wa hali ya juu, kupitia Waziri Nape Nnauye kwa ushirikiano na mwongozo wa kipekee, wazazi na familia nzima ya Julitha kwa malezi yenu kwa binti , Kamati nzima ya Miss Tanzania chini ya Mkurugenzi Hashim Lundenga (Tunashukuru sana), kwenu wanahabari hatuna maneno sahihi ya shukrani, asanteni sana," alisema Magese. Naye mshindi huyo wa tano wa Miss Afrika, Julitha Kabete, alisema anashukuru kwa ushirikiano aliupata, lakini pia nchi yake kupata thamani ya kipekee katika shindano hilo kupata nafasi tano za juu. Kabete alisema kuwa licha kutopata nafasi ya kwanza, lakini ameweza kuiwakilisha vema nchi katika shindano hilo, kwa sababu ushindani ulikuwa mkali sana. "Kwangu ni faraja kubwa kwa kuwa balozi mzuri wa Tanzania na kuweza kuwashinda wenzangu wengi ikiwemo na mwenyeji wetu ambaye hakuingia katika hatua ya tano kama ambayo mimi nimeipata nina furaha kubwa sana,"alisema Kabete. Alisema kuna mkataba mpya ambao utaingiwa kati ya Tanzania na waandaaji wa shindano hilo la Miss Africa katika kutoa ushirikiano wa ushiriki wa shindano hilo. Katika shindano hilo lililofanyika Novemba 26, mwaka huu nchini Nigeria, taji la shindano hilo lilienda kwa mnyange Neurite Mendes (23) wa Angola, aliyenyakua kitita cha dola za Marekani 25,000 sawa na sh.milioni 52 ya Kitanzania na gari jipya (brand new 2016 Ford Escape), safari maalum ya mafunzo nchini Uingereza na Ubalozi wa Mazingira– Afrika. Mshindi wa pili katika shindano hilo ni Refilwe Mthimunye wa Afrika Kusini alipata dola za Kimarekani 15, 000 ni sawa na zaidi ya sh. milioni 32, na Jencey Anwifoje kutoka nchini Cameroon, akiibuka wa tatu na kupata dola za kimarekani 10,000 sawa na zaidi ya sh.milioni 20. Shindano la Miss Afrika 2016 lilichagizwa kwa heshima ya mji wa Calabar na jimbo la Cross River, chini ya Gavana wa Cross River Profesa Ben Ayade. Kampuni tanzu ya Millen Magese (MMG) imeanzishwa kwalengo la kuibua, kuinua, kutambua na kukuza vipaji katika Bara la Afrika na ngazi ya Kimataifa. MMG imeweza kufika nchi mbalimbali barani Afrika na mwaka 2012 iliweza kuendesha shindano la kwanza ya aina yake ambapo wanamitindo wawili kutoka Tanzania walipata nafasi ya kupata mikataba nchini Afrika Kusini. Wanamitindo kutoka mashindano hayo wameweza kuendelea kufanya vizuri maonesho mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. Mwaka huo huo wa 2012 MMG kupitia mradi wa TIFEX iliwezesha wabunifu kutoka nchini kupata uzoefu na uelewa wa wiki za mitindo duniani.

TFF YATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI BRAZIL, NI ILE AJALI ILIYOTEKETEZA TIMU YA SOKA Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametuma salamu za rambirambi kwa Shirikisho la Mpira Brazil (CBF), kutokana na vifo vya wachezaji wa timu ya soka Chapecoense Real ya Brazil. Rais wa TFF Malinzi, katika salamu za rambirambi kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Brazil (CBF), Lucca Victorelli amesema ajali hiyo iliyoua watu wengi ni tukio la kusikitisha kwenye familia ya soka duniani na limetokea katika kipindi kigumu. Rais Malinzi ambaye alituma salamu hizo pia kwa mashabiki wa Chapecoense na Jumuiya ya soka na wanafamilia wengine wa nchini Brazil, amesema: “Mawazo yetu yapo kwa wahanga wa ajali hiyo, familia na jamaa zao.” Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri juzi Jumatatu kutoka Brazil kupitia Bolivia kwenda Colombia ilibeba abiria 81 wakiwamo wafanyakazi na wachezaji wa Chapecoense Real ya Brazil kabla ya kuanguka kwenye milima ya Colombia. Wachezaji hao wa Chapecoense Real ya Brazil walikuwa wakisafiri kwenda kucheza mechi ya fainali ya michuano ya ubingwa wa Kombe la Amerika ya Kusini (Copa Sud Americana). Walikuwa ni miongoni mwa abiria 81. Michuano hiyo ni ya pili kwa ukubwa katika Bara la Amerika ya Kusini, iliyotarajiwa kuchezwa leo Jumatano Novemba 30, 2016 ambako Chapecoense Real ingecheza dhidi ya Atletico Nacional ya Colombia. Ndege hiyo ilikuwa imebeba wachezaji wa timu ya Chapecoense Real ya Brazil, awali ilitoa taarifa ya hali ya hatari iliyosababishwa na hitilafu kwenye mfumo wa umeme, na hatimaye kuanguka muda mfupi baadaye karibu na mji wa Medelin. Taarifa za vifo hivyo, zimethibitishwa na Mkuu wa Mamlaka ya Anga ya Brazil, Alfredo Bocanegra aliyesema walionusurika ni Watu watano wakiwamo wachezaji watatu wa Chapecoense na wafanyakazi wawili wa ndege hiyo.

Wacha nifunguke Uamuzi wa kutumia busara badala ya sheria na kanuni TFF mnautoa wapi? Huu utaratibu wa kutumia busara katika kufanya maamuzi ya kisheria na kanuni tumeutoa wapi? Taratibu zinajulikana, sheria zipo, kamati husika ipo, kilichokuwa kinatakiwa ni kulishughulikia jambo hili kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni kwa kuzingatia ushahidi wa pande zote mbili ili upande wenye haki upewe haki yake. Kuna faida mbili kama kamati ingesimama katika sheria kuliko kuipeleka kesi hii kishkaji na siasa za Simba na Yanga. Faida ya kwanza kama kesi hii ingeamuliwa kisheria ni kuijengea heshima na imani TFF na mamlaka husika kwa kusimama kwenye haki pasipo kuyumba na kutoa fundisho au angalizo kwa wengine kwamba taasisi haiyumbishwi imesimama kwenye mstari. Jambo la pili ni kutengeneza mazingira ya kuwasaidia wachezaji wenyewe kwamba hata kama wanafanya ujinga wa kufanya udanganyifu na kusaini timu mbili au kusaini timu nyingine wakati bado mikataba yao na timu nyingine ipo hai watakua wakijua lazima watakabiliwa na adhabu bila kujali ni wachezaji wa Simba au Yanga. Lakini inapofika wakati TFF inatoa nafasi kwa vilabu kumalizana nje ya sheria wanakuwa hawatatui tatizo la muda mrefu, vipi mambo hayo yakifanywa na vilabu kama Ruvu Shooting na Mbao FC? Msimu ujao huenda Simba wakamsajili mchezaji wa Yanga kimagumashi TFF haitakuwa na meno ya kuiadhibu Simba moja kwa moja kwasababu Yanga walipofanya hivyo TFF ilitoa nafasi kwa vilabu kumalizana kisela. Jana afisa habari wa TFF Alfred Lucas aliutangazia umma wa watanzania kwamba, kesi hiyo imerudishwa kwenye kamati ya sheria na hadhi za wachezaji kwa ajili ya kufanyiwa uamuzi, TFF imeiagiza Simba kupeleka mkataba halali waliosainiana kati ya Simba na Hassan Ramadhani Kessy pamoja na ushahidi unaothibisha kwamba Simba walikuwa wanamlipa Kessy hususan katika miezi mitatu ya mwisho. Sasahivi kesi imegeuka, mwanzo Simba walilalamika kuwa Kessy alivunja mkataba kwa kuanza kuitumikia Yanga wakati bado alikuwa na mkataba halali na klabu ya Simba. TFF badala ya kuamua Kessy ya msingi sasahivi inataka kujiridhisha kama Kessy alikuwa akilipwa mshahara au la! Mbona Kessy hakufungua kesi ya kuidai Simba? Kwahiyo, kama mchezaji akiwa anaidai klabu mishahara inabidi asajiliwe na klabu nyingine bila kufuata taratibu? Kwa mujibu wa taarifa za Simba, Kessy alibakiza siku chache ili mkataba wake na Simba umalizike, lakini hiyo haimaanishi mchezaji alitakiwa avae jezi za Yanga, kusafiri au kuhusika moja kwa moja na shughuli za Yanga ilibidi asubiri hadi mkataba wake umalizike. Baada ya Yanga kuona wamefanya kosa huenda Kessy aliwaambia makataba wake na Simba umemalizika lakini wao hawakujiridhisha, wanatafuta sehemu ya kusawazisha ndiyo maana wanaomba ushahidi (salary slip au bank statement) wa malipo ya mishahara ya Simba kumlipa Kessy. Sasa kama Simba walikuwa wanamlipa Kessy kishkaji kwa kutoa pesa mfukoni bila maandishi watashindwa kwenye kesi hii kwasababu wakishindwa kuthibitsha kwamba walikuwa wanamlipa Kessy kwa zaidi ya miezi mitatu, basi moja kwa moja mkataba utakuwa ulivunjwa na Simba wenyewe. Ngoja tuendelee kujionea sarakasi za Simba na Yanga kwenye soka la Tanzania huku jaji wao akiwa ni kipofu.

DONEDEAL: Ngasa kasaini Mbeya City Picha inayo-trend kwa sasa kwenye mitandao ya kijamii ni ya Mrisho Ngasa na afisa habari wa Mbeya City Dismas Ten ambayo inaashiria tayari nyota huyo wa zamani wa Yanga ameshakamilisha deal na ‘wagonga nyundo wa Mbeya’ Mbeya City. Mwezi Septemba mwaka huu Ngasa alijiunga na Fanja FC inayoshiriki ligi kuu nchini Oman (Oman Professional League) ikiwa ni wiki tatu tu, baada ya kuvunja mkataba na klabu ya Free State Stars ya South Africa. Nyota huyo wa zamani wa vilabu vya Kagera Sugar, Yanga, Azam FC na Simba vyote vya VPL hajadumu Oman na hatimaye amerejea tena nchini na kusajiliwa na klabu ya Mbeya City ambapo ataungana na kocha wake wa zamani Kinna Phiri aliyemsajili kutoka Yanga kwenda Free State Stars kabla ya kocha huyo kutimuliwa kufatia mfululizo wa matokeo mabovu. Afisa habari wa Mbeya City Dismas Ten ame-post picha kwenye ukurasa wake wa Instagram akiwa pamoja na Mrisho Ngasa na kuandika maneno yanosomeka: “Mnapokamilisha jambo kutakiana heri ndio uungwana. Kila la heri anko @mrisho_ngasa_17.” Habari za Ngasa kujiunga na Mbeya City zilianza tangu aliporejea nchini akitokea South Africa baada ya kuvunja mkataba na Free State lakini ghafla akaibukia Oman na kusajiliwa na Fanja FC siku chache baada ya klabu hiyo kumsajili mtanzania mwingine Danny Lyanga mshambuliaji wa zamani wa Simba. Jana jioni zikaenea tena habari kwamba Mbeya City wameshakamilisha usajili wa Ngasa. Lakini uongozi wa klabu hiyo haukuwa tayari kuthibitisha badala yake ukasema utatoa taarifa rasmi, mwisho wa siku raundi ijayo ya VPL Ngasa atakuwa miongoni mwa wachezaji watakaokipiga Mbeya City.